Waandishi wa habari wafundwa

WAANDISHI wa Habari nchini wameshauriwa kuandika habari kwa kutumia vyanzo mbalimbali ili iweze kukamilika na kuwa nzuri, inayowawezesha wasomaji na wasikilizaji kuendelea kuifuatilia.
Ushauri huo umetolewa na mhadhiri msaidizi kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), Swaum Manengelo alipozungumza na HabariLeo katika Maonesho ya 47 ya Biashara ya Kimataifa yanayoendelea Dar es Salaam.
“Tunavyovichunguza ni muhimu kuzingatia haya kwa sababu tunapata malalamiko kwa wasomaji na watazamaji kwamba waandishi wa Habari hawafanyi kazi zao kama inavyotakiwa kufanya na ndio maana kuna vigezo vilivyowekwa kuhakikisha mwandishi wa Habari anapita kule kwa lengo la kumridhisha msomaji,” amesema.
Amesema katika utafiti walioufanya wa mradi wa Yearbook kwa vyombo mbalimbali vya Habari, imebainika habari nyingi zimekuwa na chanzo cha Habari kimoja.
“Chanzo cha Habari kimoja hakikamilishi Habari ni mazingatio ya muhimu kwa waandishi wa Habari kuhakikisha kwamba wanawafikia walengwa wote ili Habari iwe nzuri,” amesema.
Amesema katika ripoti ya mradi huo wamekuwa wakiangalia hali ya uripoti wa Habari nchini Tanzania kwa kuangalia magazeti, redio za kitaifa, redio za kimkoa pamoja na televisheni.
Pia amesema wanaangalia vyombo vya Habari vinavyoripoti katika misingi mbalimbali ikiwemo maadili ya kiuandishi ikiwemo kupata maoni na mitazamo ya wananchi.
mwisho