Waandishi wapewa somo kuisaidia serikali

Waandishi wapewa somo kuisaidia serikali

WAANDISHI wa habari nchini wametakiwa kuisaidia serikali kwa kukosoa mambo yote yanayofanywa kinyume na utaratibu, badala ya kusifia kila jambo hata kama haliko sawa.

Mtafiti wa Masuala ya Habari kutoka Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Shule Kuu ya Uandishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma (SJMC), Abdalah Katunzi ambaye ni Mratibu wa Mradi wa Yearbook, amesema hayo wakati wa uzinduzi wa Wiki ya Utafiti na Ubunifu kwa shule hiyo ya uandishi wa habari.

Amesema kwa kufanya hivyo kutamsaidia Rais Samia Suluhu Hassan katika ufuatiliaji wa utendaji serikalini, kwani amewahi kusema kuwa kuna mchwa wanakula fedha za serikali, hivyo kwa kufichua maovu kutasaidia mambo ya nchi kwenda sawa.

Advertisement

“Kazi ya vyombo vya habari sio kusifia tu, yanapotokea mambo ambayo hayako sawasawa tunapaswa kusema. Asilimia 3.7  ya kazi zote za mwaka jana na mwaka huu ndio zimekosoa serikali. Kuna haja ya kuangalia namna ya kuisaidia serikali,” amesema.

Amesema ripoti ya mwaka jana iliyozinduliwa katika mradi wa kuboresha uripoti wa vyombo vya habari nchini imeonesha kuwa kwa Tanzania asilimia 60 kuanzia mwaka 2017 ya kazi zote zinazozalishwa na vyombo vya habari ni habari za matukio, zinazohusu warsha, semina, mikutano na bunge.

 

Mratibu wa Utafiti na Ubadilishaji Maarifa, Shule Kuu ya Undishi wa Habari na Mawasiliano kwa Umma(SJMC), Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Egbert Mkoko akizungumza na wanafunzi wa vyuo vya habari.

“Na habari ambazo waandishi wanakwenda kutafuta wenyewe ni asilimia 40. Watafiti tunasema hii sio hali nzuri kwa tasnia ya habari kwa sababu tunakuwa tunawategemea watu wengine watupatie habari na hao wana ajenda zao. Nasi tunafanya kazi ya kubeba ajenda zao kupeleka kwa wananchi,” amesema.

Naye Mratibu wa Mradi wa Norpart, Dk Eva Solomon kutoka chuoni hapo ameelezea lengo la mradi huo kuwa ni kuboresha mafunzo ya uandishi wa habari kwa kutumia mbinu mbalimbali na teknolojia, pia kutumia uzoefu wa walimu wanaofundisha waandishi wa habari. 

Awali Mratibu wa Utafiti na Ubadilishaji Maarifa SJMC, Dk Egbert Mkoko amesema shule hiyo ya uandishi imezindua maonesho ya wiki ya utafiti ambayo yatafanyika kwa siku tatu kuanzia jana mpaka kesho.

“Maonesho haya yanakusudia kuonesha tafiti mbalimbali zilizofanywa na zinazoendelea kufanywa na shule kuu, ikiwa ni pamoja na kazi za ubunifu katika taaluma ya habari sambamba na machapisho ambayo yapo kwenye majaridi ya kitaaluma kuhusu taaluma ya habari,” amesema.