Waanza kulipia maegesho Muhimbili

HOSPITALI ya Taifa Muhimbili (MNH) imenza rasmi utaratibu wa kulipia maegesho katika hospitali hiyo.

Ofisa Habari wa Muhimbili, Aminiel Eligaesha akizungumza na HabariLEO amesema lengo ni kupunguza msongamano wa magari katika hospitali hiyo, utaratibu huo umeanza rasmi juzi Agosti Mosi, baada ya kumaliza wiki mbili za majaribio.

“Kipindi cha majaribio kimeisha, hivyo tangu tarehe moja mwezi wa nane atakayeingia na gari kuanzia dakika moja hadi dakika 30 ni bure hatalipia, lakini ikizidi hapo ndipo atalipa Sh 1,000 na baada ya saa nne kupita atalipa Sh 500 kwa kila saa itakayoongezeka,” amesema.

 

Amesema mgonjwa atakayefika hospitalini akiendesha gari na ikatokea akalazwa, hatatakiwa kulipia gharama za maegesho. Kundi lingine ambalo halihusiki na malipo ya maegesho ni la wafanyakazi wa hospitali hiyo.

“Utaratibu huu wa maegesho ya kulipia unakuja na faida mbili. Mosi ni kuiingizia hospitali kipato na pili  ni kudhibiti msongamano wa magari,” amesisitiza.

Pia  amesema utafiti uliofanyika kwa mwezi mzima ulibaini kwa siku yanaingia magari kati ya 3,000 na 3,500.

Amesema inapofika muda wa watu kwenda kuona  wagonjwa huwa kuna magari zaidi ya 1,000 na Muhimbili kuna jumla ya maegesho 240 na hayatumiwi na wanaokwenda kuwatazama wagonjwa pekee.

“Tulichogundua ni kwamba, watu wanaingia na magari asubuhi, wanayapaki hapa kwa sababu kuna ulinzi halafu wanatoka wanaenda kufanya kazi mjini na jioni wanakuja kuyachukua,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button