RAIS wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi amesema hayupo tayari kuwalinda wabadhirifu wa mali za umma.
Ameahidi Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) ya mwaka 2021/2022 itasomwa hadharani Jumamosi na watakaohusika watachukuliwa hatua za kisheria.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Unguja jana, alisema huo ndio msimamo wake na yeye ndiye aliyeanzisha utaratibu wa kusomwa kwa ripoti hiyo hadharani mara alipoingia madarakani miaka miwili iliyopita.
Alisema amefanya hivyo kwa ajili ya kuweka wazi utendaji wa watumishi wa umma waliokabidhiwa majukumu ya utendaji ambapo lengo ni kujenga utawala bora na nidhamu ya fedha za umma.
Dk Mwinyi alitoa ufafanuzi baada ya kuulizwa kwamba tayari amekabidhiwa ripoti ya CAG Ikulu wiki mbili zilizopita lakini haijasomwa hadharani kama ulivyokuwa utaratibu wa awali ambao ameuanzisha alipoingia madarakani kusomwa taarifa hiyo.
Alisema zipo hatua mbili zinazopaswa kuchukuliwa katika utekelezaji wa ripoti ya CAG ikiwemo za kiutawala ambazo ni kumwondoa mhusika katika nafasi yake.
Aidha, aliutaja utaratibu mwingine ambao ni kushtakiwa kwa kosa la jinai kutokana na tuhuma za ubadhirifu wa mali ya umma zinazomkabili mhusika.
Alisema zipo hatua nyingine ambapo ripoti hiyo kupelekwa baraza la wawakilishi na kushughulikiwa na kamati ya hesabu ya mashirika ya umma ya baraza la wawakilishi ambayo tayari imesomwa baraza la wawakilishi baada ya spika kukabidhiwa.
Alisema tayari wapo watendaji wa ngazi za juu serikalini wamechukuliwa hatua za awali ikiwemo kusimamishwa kazi na kuondolewa katika nafasi zao walizokuwa wakishikilia.
Dk Mwinyi alisema serikali yake imedhamiria kuleta maendeleo ikiwemo kutekeleza mradi wa ujenzi wa bandari ya Mangapwani Mkoa wa Kaskazini Unguja katika hadhi ya kuwa bandari shirikishi.
Alisema wanakusudia katika mradi huo kuwepo maeneo ya makontena, maeneo ya kuhifadhi mafuta na gesi pamoja na maeneo huru ya uchumi katika uwekezaji.
Alisema serikali bado inaendelea kutafuta wawekezaji watakaowekeza eneo hilo na kuufanya mji wa Mangapwani kuwa mji wa bandari.
Alisema wawekezaji kutoka Oman bado hawajajiondoa na kazi ya kutafuta wawekezaji wengine zaidi kutekeleza mradi huo mkubwa zinaendelea.
Aliwataka wananchi kuwapuuza wapinzani ambao wameanza kuchanganyikiwa na kasi ya kuleta maendeleo inayofanywa na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) Awamu ya Nane katika sekta mbalimbali ikiwemo miundombinu pamoja na ujenzi wa barabara zinazokwenda mjini na vijijini.
Alisema katika mwaka wa kwanza wa uongozi wake wapinzani walikuwa wakihoji utendaji wake na kutoa mfano wa serikali kushindwa kutekeleza miradi ya maendeleo.
Akizungumzia safari yake ya Qatar ambapo alihudhuria mkutano mkubwa wa kimataifa wa biashara na uwekezaji wa Doha, akimwakilisha Rais wa Jamhuri ya Muungano, Samia Suluhu Hassan, alisema ulikuwa wa mafanikio makubwa.
Alisema baadhi ya mashirika makubwa ya kimataifa yameonesha nia ya kuwekeza katika sekta mbalimbali kuu ikiwemo uchumi wa buluu katika utalii, mafuta na gesi pamoja na uvuvi.
Alisema Qatar ni maarufu katika uzalishaji wa mafuta na gesi ambapo kampuni za huko zimeonesha nia kuja kuwekeza zaidi katika masuala ya utafiti, uzalishaji wa mafuta na masuala ya fedha.
Aidha, alisema kupitia Mamlaka ya Uwekezaji (ZIPA) imetangaza vivutio vya uwekezaji ikiwemo katika miradi ya uwekezaji katika visiwa vodogo vidogo vilivyopo Unguja na Pemba.