Wabunge 95% waikubali bajeti, Rais apongezwa

WABUNGE wamepitisha kwa kishindo Bajeti ya Serikali Kuu kwa mwaka 2023/24 baada ya asilimia 95 ya wabunge waliopiga kura kupiga kura ya maamuzi ya Ndiyo. Juni 15, mwaka huu, serikali iliwasilisha bungeni Bajeti ya Mapato na Matumizi ya Serikali ya Sh trilioni 44.39 ikiwa imeongezeka kwa asilimia 7 kutoka Sh trilioni 41.5.

Bajeti hiyo imepitishwa na wabunge 354 waliopiga kura za ndiyo wakiwamo wabunge watatu wa upinzani wakiiunga mkono. Wapinzani waliopiga kura ya Ndiyo ni wabunge wa viti maalumu wa Chadema, Salome Makamba na Nusrat Hanje na mmoja wa Chama cha ACT-Wazalendo, Seif Salim Seif.

Hatua hiyo iliibua shangwe kwa wabunge na kuwapigia makofi, kutokana na kufanya uamuzi tofauti na mategemeo ya wabunge wa kutoka vyama vya upinzani kupiga kura ya kutokuwa na uamuzi au ya Hapana. Akizungumza kwenye viwanja vya bunge, Salome alisema:

“Nimepiga kura ya ndiyo kwa sababu ninataka serikali iende ikatekeleze miradi ya maendeleo iliyowaahidi wananchi, bado muda wa kupima haujafika, hivyo tumkopeshe imani Mheshimiwa Rais tuone kama atatulipa imani.”

Kabla ya kupiga kura hizo, Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson aliwakumbusha wabunge kifungu cha Katiba Ibara ya 90 (11) B ambayo inasema Rais hatakuwa na uwezo wa kulivunja bunge wakati wowote isipokuwa tu (b) kama bunge litakataa kupitisha bajeti iliyopendekezwa na serikali.

“Na kanuni yetu ya 126 inataka mbunge aitwe jina lake na aitike na kupiga kura ile ambayo yeye anaona inafaa,” alisema Dk Tulia.

Bunge lina wabunge 393, lakini wanaopaswa kupiga kura ni wabunge 392 ukiondoa kura ya Spika ambaye yeye anapiga kura ya uamuzi kama kura zimefungana.

Wakati anatangaza matokeo, Dk Tulia alisema wakati wa kupiga kura bungeni wabunge waliokuwa ndani ya ukumbi walikuwa 374 na 18 hawakuwepo.

“Kura za Hapana ni sifuri, kura ambazo hazikuwa na uamuzi ni kura 20 na kura za Ndiyo ni 354. Waheshimiwa wabunge, kwa muktadha huu, Bajeti ya Serikali kwa Mwaka 2023/24 imepitishwa kwa kura 3, sawa na asilimia 95 ya wabunge waliopiga kura,” alisema.

Aliongeza: “Nampongeza Rais Samia ambaye ameleta bajeti yake hapa kama kiongozi wa serikali na bunge limepitisha.” Aidha, katika upigaji kura huo, Mbunge wa Jimbo la Lulindi, Issa Mchungahela (CCM) alijikuta anapiga kura wa mwisho baada ya kuwa nje wakati ameitwa jina kupiga kura.

Vicheko viliibuka bungeni baada ya Mchungahela kuibuka na kuomba mwongozo wa Spika ili apige kura wakati Katibu wa Bunge, Nenelwa Mwihambi akiwa anaenda kuzihesabu. Wakati anaomba kupiga kura mbunge huyo alimweleza Spika kuwa alikwenda nje kutokana na matatizo ya tumbo.

Dk Tulia alimruhusu apige kura hiyo na alimuagiza katibu wa bunge amuite jina ili mbunge huyo atumie haki yake ya kupiga kura kwa bajeti.

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button