CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Iringa kimewatolea uvivu wawakilishi wake wa wananchi wanaokacha kushiriki vikao mbalimbali vya chama hicho kwa madai ya kuwa na udhuru kikisema wanajiweka katika mazingira magumu ya kwenda nao pamoja katika chaguzi zinazokuja.
Kimetoa msimamo huo leo katika kikao chake maalumu ambacho mgeni wake rasmi alikuwa Katibu wa NEC Organizesheni, Issa Haji Ussi (Gavu) kilichofanyika katika ukumbi wa Ihemi nje ya Iringa na kushirikisha wajumbe zaidi ya 700 wa halmashauri kuu za wilaya zote za kichama za mkoa huo.
Wawakilishi ambao hawakuwepo katika kikao hicho wakati tamko hilo likitolewa ni pamoja na Mbunge wa Iringa Mjini Jesca Msambatavangu, wa Mafinga Mji Cosato Chumi, Kilolo-Justin Nyamoga, Isimani-William Lukuvi, na Mufundi Kaskazini-Exaud Kigahe.
Wengine ambao hawakuhudhuria kikao hicho ni wabunge wote watatu wa Viti Maalumu wanaowakilisha Mkoa wa Iringa akiwemo Ritta Kabati, Rose Tweve na Nancy Nyalusi.
Akiongea kwa uchungu huku akipigiwa makofi na wajumbe wao wakiwemo wabunge wawili waliohudhuria Jackson Kiswaga wa jimbo la Kalenga na David Kihenzile wa Mufindi kusini, Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa Salim Asas alisema; “Hiki ni kikao muhimu sana na sisi kama viongozi wa mkoa tumekichukua kwa kwa umuhimu mkubwa.”
“Kuna ujumbe nataka muwapelekee wale wote wanaopata udhuru, maana nasikia kuna watu muhimu wamepata udhuru wa kuhudhuria kikao hicho ambacho moja kati ya ajenda ni kujua hao wanaopata udhuru uchaguzi wa 2025 watavukaje.” alisema.
Akitoa maelekezo kwa wajumbe wa kikao hicho Asas alisema mkibahatika kuonana nao; “Waambieni tulikaa kule Ihemi kuangalia kwamba 2025 mtavukaje. Sasa kwasababu walipata udhuru, na wanajua 2025 ninyi mtajitoa kuwapigania, waulizeni na ninyi mkipata udhuru hiyo 2025 wataweza vipi kupita.”
Akipigilia msumari wa moto katika msimamo huo, Gavo alimuagiza Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa Daudi Yasin kusimamia kidete jambo hilo akisema inashangaza kuona mkoa una viongozi wanaotafuta kujichoma mikuki wao wenyewe kwa kutoshiriki vikao vnavyojadili hatma yao.
“Haifurahishi kuona wale tunaowatengenezea maandalizi ya kuchaguliwa wanatukimbia. Waiteni na wasemeni. Kikao hiki kilipangwa muda na taarifa wanazo, kutokuwepo kwao kwa visingizio mbalimbali ni kudharau vikao vya chama. Waambie ndani ya CCM hakuna kiongozi wa kudharau chama,” Gavo alisema.
Aidha Gavo ametoa wito kwa wajumbe walioshiriki kikao hicho kujipanga kwa uchaguzi wa serikali za mitaa mwakani kwa kuhakikisha vijana na wanawake wanapewa nafasi kubwa zaidi katika uchaguzi huo.
“CCM ni chama kinachojitofautisha na vyama vingine kwasababu kubwa mbili moja ndio chama tawala lakini pili ndicho chama kilichopewa dhamana na wananchi kuwaletea maendeleo. Kwahiyo tukachague viongozi waadilifu, wazalendo na wenye kiu inayokidhi matamanio ya wananchi katika kushughulikia changamoto zao,” alisema.
Awali Asas alizungumzia mikakati ya kukiimarisha chama hicho akisema mpango wao wa kuhakikisha kinakuwa na ofisi katika kata zote 107 unatekelezwa ndani ya miaka minne ijayo.
“Makubaliano yetu katika kamati ya siasa ya mkoa ni kuanza kuzisaidia zile kata zilizoanzisha ujenzi na zenye viwanja na baadhi ya vifaa vya ujenzi. Kwahiyo zile zisizo na sifa hizo zichangamke,” alisema na kuhimiza ajenda yake ya siasa na uchumi kwa kuzikumbusha kata hizo kuwa na miradi itakayowaingizia kipato.
Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Halima Dendego alitoa taarifa ya utekelezaji wa Ilani ya CCM katika kusukuma maendeleo ya mkoa huo huku Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Iringa, Daudi Yasin akizungumzia nia njema na kasi kubwa ya Rais Dk Samia Suluhu Hassan ya kuwaleta watanzania maendeleo.
“Sisi wote ni mashahidi na mwenye macho haambiwi tazama. Kwa kazi anayofanya Mama Samia tuahidi hakuna namna yoyote tunaweza kumuangusha,” alisema katika kikao hicho kikubwa kufanyika mkoani Iringa kutathmini hali ya kisiasa na kuweka mikakati ya kushughulikia changamoto zake.