WABUNGE wa Bunge la Jumuiya ya Afrika Mashariki (EALA) kutoka Tanzania wametoa rai kwa wanasiasa na wananchi kutotumia kauli zinazotishia umoja wa kitaifa na muungano katika kujadili mchakato unaoendelea wa makubaliano kati ya Serikali ya Tanzania na Dubai kwenye ushirikiano wa uendelezaji wa bandari nchini.
Aidha, wamemuomba Msajili wa Vyama vya Siasa, kufuatilia kwa makini suala hilo na endapo atabaini kuna ukiukwaji wa sheria hatua stahiki zichukuliwe.
Akizungumza na waandishi wa habari jana mjini hapa, Mbunge Dk Abdullah Makame alisema hivi karibuni kumeibuka maneno kati ya wanasiasa na wananchi kupitia mitandao ya kijamii kuhusu uwekezaji wa bandari baada ya serikali kuichagua Kampuni ya Dubai ya Port World (DPW)
Alisema kauli zinazotolewa na baadhi ya wanasiasa na wananchi zinaleta ubaguzi katika muktadha mzima wa muungano ulioasisiwa na Mwalimu Julius Nyerere na Abeid Amani Karume.
Alisema wabunge hao wameamua kutoa karipio juu mjadala unaochukua tafsiri ya ubaguzi kwa vigezo vya eneo ambalo watanzania wanatokea au kwa kutumia dini zao.
“Mjadala unaochukua taswira ya ubaguzi hauna afya kwa mustakabali wa taifa na unaweza kuhatarisha utulivu tulionao kama taifa, usipomalizwa mara moja una uwezekano wa kuzalisha ladha chachu za Muungano na tunapaswa kulinda hususan kwa viongozi ambazo nafasi zetu tumezipata kutokana na vyama vya siasa ambavyo vimesajiliwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.
Naye Mbunge Machano Ali Machano alisema EAC ni ya watu wenye umoja hivyo ni lazima umoja ulindwe kwani kuna watu wanaona wivu.
“Waafrika wote ni ndugu tusibaguane, sisi ni wamoja twende pamoja kwa ajili ya kuimarisha Muungano ikiwemo umoja wetu ambao baadhi ya watu wanatuonea wivu hivyo tuendelee kulinda muungano wetu,” alisema.
Alitoa rai kwa viongozi wote wa kisiasa, wa dini na wengineo pamoja na wananchi kuimarisha umoja, amani, upendo na utawala bora nchini ili kukemea kila aina ya ubaguzi.
Naye Mbunge Nadra Juma Mohammed alisema wananchi wanapaswa kuwaamini viongozi na serikali ili kutoa muktadha wa nchi kwa sababu mchakato wa jambo hilo bado upo bungeni hivyo wanapaswa kuwa watulivu.