SERIKALI imeshauriwa kuanzisha mpango wa kuwapa wazee wote pensheni ikiwa ni hatua ya kuthamini mchango wao kwa taifa.
Ushauri huo ulitolewa jana na wabunge waliochangia mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Mbunge wa Muleba Kaskazini, Charles Mwijage (CCM) alisema pensheni inayotolewa kwa watu waliowahi kuitumikia serikali ni ndogo kwa kuzingatia thamani ya fedha.
“Watu wana matatizo kama vile magonjwa…lakini wakienda serikali, bima za afya haziwasaidii,” alisema Mwijage na kuiambia serikali kuwa isiwe na wasiwasi na kiwango cha kuwalipa kwa sababu ni wachache.
Mbunge wa Jang’ombe, Ali Hassan King alisema wapo wazee waliostaafu lakini pensheni yao ni ndogo. Aliomba serikali kuunda kikosi kasi kufuatilia pensheni zao kwa kile alichosema sheria iliyoundwa haizingatiwi.
Mbunge wa Muleba Kusini, Dk Oscar Kikoyo (CCM) alisema wapo wazee wengi waliotumikia taifa kwa maana ya kuchangia pato ambao serikali haina budi kuthamini mchango wao.
“Tuna wazee waliokuwa wakulima na walichangia pato, ni wengi na kusema kweli, hotuba ya Waziri Mkuu amewaongelea…wanahitaji kutambuliwa si kwa maneno bali kwa kupewa pensheni hata ndogo,” alisema Dk Kikoyo.
Aliongeza: “Tunataka yanayofanyika Zanzibar, pia na wazee wa Tanzania Bara waangaliwe, wametumikia taifa katika nyanja mbalimbali kama vile kilimo, mifugo, uvuvi.”
Katika hatua nyingine, wabunge pia walizungumzia migogoro ya ardhi baina ya wananchi na baadhi ya taasisi za serikali na kutaka serikali itafute suluhisho haraka kwa maslahi ya wananchi.
Mbunge wa Ngara, Ndaisaba Ruhoro (CCM) alihoji sababu za baadhi ya taasisi kutotaka uchimbaji wa madini kufanyika kwenye hifadhi wakati Rais Samia Suluhu Hassan alishafafanua juu ya hilo.