WABUNGE kutoka nchini Uganda wapo nchini kwa ajili ya kujifunza namna sheria ya ndoa inavyotekelezwa hapa nchini, changamoto zilizopo kwa sasa na namna wanavyojipanga kuzitatua.
Mwenyekiti wa Chama cha Wabunge Wanawake nchini Uganda, Sara Opendi amesema hayo baada ya kukutana na Menejimenti ya Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzamia ( LRCT).
Opendi amesema wamekuja kujifunza eneo hilo kwa sababu kwa serikali ya Uganda ipo kwenye mchakato wa kuandaa muswada wa sheria ya ndoa, hivyo wapo Tanzania kwa ajili ya kupata uzoefu kutoka nchi mbalimbali zinazotekeleza sheria hiyo ikiwemo Tanzania na Zimbabwe.
“Uganda kuna ndoa za aina nyingi ambapo muswada huo unategemewa kugusa jamii yote huku kama ambavyo Tanzania ilivyofanya kwa kuzingatia ndoa za kidini, ndoa za kimila na ndoa za serikali,” amesema.
Akielezea uzoefu kuhusu sheria ya ndoa, Katibu Mtendaji Tume ya Kurekebisha Sheria Tanzania. Griffin Mwakapeje amesema tume inatambua ndoa kama taasisi ambayo haina budi kulindwa kwa lengo la kuwa na Taifa bora.
“Ni kutokana na hilo sheria inaweka masharti mbalimbali yakiwemo ya mke na mume kuishi pamoja kwa muda wa uhai wao, aina za ufungaji wa ndoa zinazotambuliwa,
“Nafasi ya mwenza wa ndoa kutoa ridhaa wakati wa kuuza mali za ndoa; masharti ya talaka; na masharti ya dhana ya ndoa baada ya wahusika kuishi pamoja bila kuisajili ndoa hiyo,” amesema.
Mwakapeje amesema uzoefu wa Tanzania unaonesha sheria moja ya ndoa ilipatikana mwaka 1971 baada ya maridhiano ya wanajamii wote na kuzifuta sheria nyingi zilizokuwepo ambazo zilikuwa zinasimamia masuala ya ndoa.
Amesema hivyo Uganda wanaweza kujifunza Tanzania ili na wao pia pamoja na mambo mengine waweze kuwa na sheria moja ya ndoa tofauti na ilivyo sasa.