Wabunge wa zamani waibukia uenyekiti CCM wilaya

BAADHI ya wabunge waliokuwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa nyakati tofauti ni miongoni mwa wanachama wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) walioteuliwa kuwania uenyekiti wa chama hicho ngazi ya wilaya Tanzania Bara na Tanzania Zanzibar.

CCM juzi ilitangaza kupitisha wanachama wake kuwania uenyekiti wa wilaya katika wilaya 168 za kichama katika uchaguzi uliopangwa kufanyika Oktoba Mosi na Oktoba 2, mwaka huu katika mikoa yote nchini.

Kwa mujibu wa Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya CCM, Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka, NEC chini ya Mwenyekiti wa CCM Taifa, Rais Samia Suluhu Hassan imefanya uteuzi huo juzi kwenye Makao Makuu ya CCM, White House jijini Dodoma.

Baada ya kikao hicho, Shaka alitoa majina ya wana CCM walioteuliwa kuwania uenyekiti katika wilaya 168 za kichama ikionesha kuwapo kwa vigogo waliowahi kuwa wabunge na wengine nafasi za juu katika chama.

Orodha hiyo inaonesha kuwa baadhi ya wilaya, wameteuliwa wagombea wanne na wilaya nyingine wagombea watatu, huku pia wenyeviti wa zamani wakiteuliwa katika baadhi ya wilaya na wengine hawamo.

Miongoni mwa wabunge wa zamani walioteuliwa ni Anatory Choya wa Biharamulo mkoani Kagera ambaye atawania uenyekiti wa wilaya hiyo akipambana na Robert Malulu, Lucas John na Pili Makunenge.

Mbunge wa zamani wa Kigoma Vijijini, Halimenshi Mayonga ameteuliwa Wilaya ya Kigoma Vijijini ambako atakabiliana na Deusidedth Alphonce na Jeremiah Bayaga kuongoza CCM wilayani humo.

Mbunge za zamani wa Masasi na Viti Maalumu Mkoa wa Mtwara, Mariam Kasembe ameteuliwa kuwania uenyekiti wa CCM Wilaya ya Masasi akiteuliwa pamoja na Arafati Hassani, Edward Mwavele na Margaret Malenga.

Mwingine ni aliyekuwa Mbunge wa Ludewa, Stanley Kolimba ambaye ameteuliwa kuwania uenyekiti katika wilaya hiyo na atachuana na Thobias Lingalangala, Teopista Mhagama na Silvester Mgina.

Katika orodha hiyo yumo pia aliyekuwa Mbunge wa Kibiti, Abdul Marombwa aliyeteuliwa katika wilaya hiyo akiwa sambamba na Abdallah Mpili na Juma Ndaruke.

Kigogo mwingine aliyeteuliwa ni Katibu wa zamani wa CCM wa mikoa kadhaa nchini ikiwamo ya Pwani na Kusini Unguja, Sauda Mpambalyoto aliyepitishwa katika Wilaya ya Kibaha Mjini ambako atakabiliana na Bundala Maulid, Mwajuma Nyamka na Abdallah Mdimu.

Katika Wilaya ya Mlele mkoani Katavi, walioteuliwa ni Wolfugang Mizengo Pinda, Erick Kagusa na Jojina Kasamya wakati katika Wilaya ya Musoma Mjini mkoani Mara, yumo kada wa siku nyingi, Daudi Misango atakayevaana na Benitha Kishobera na Magiri Maregesi.

Kwa mujibu wa Shaka, CCM imeweka historia baada ya wanachama zaidi ya milioni mbili kujitokeza kutumia haki ya kidemokrasia kuomba kuteuliwa kugombea nafasi za uongozi katika uchaguzi wa ndani unaoendelea nchini.

Shaka amesema kwa idadi kubwa ya wagombea waliojitokeza, imedhihirisha kwamba CCM ipo imara, ina nguvu na kuungwa mkono.

“Katika historia ya Chama Cha Mapinduzi kwa mara ya kwanza mwaka huu wa uchaguzi 2022, wana CCM wengi wamejitokeza kuomba nafasi mbalimbali za uongozi ndani ya chama, haijapata kutokea,” alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button