Wabunge wacharuka ripoti ya CAG
MTIFUANO umetokea bungeni baada ya wabunge kucharuka kuhusu ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG), huku Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba akikaliwa kooni na Spika wa Bunge, Tulia Ackson baada ya Mbunge wa Simanjiro Christopher Ole Sendeka kuomba mwongozo wa Spika.
Awali Mbunge wa Viti maalum, Esther Matiko akichangia ripoti hiyo, alihoji manung’uniko yaliyotolewa na Rais Machi 29, 2023 kuhusu manununuzi ya ndege mpya ya mizigo ya Air Tanzania, ambayo kuna ongezeko la fedha kinyume na makubaliano.
Awali malipo ni Dola milioni 37, lakini ‘invoice’ iliyopelekwa serikalini ni Dola za Marekani milioni 86 kwa madai ya kuwa gharama ya vifaa imepanda.
Hata hivyo katika majibu yake Waziri wa Fedha Mwigulu Nchemba alisema malipo yote yanayofanywa yanaidhinishwa na Rais.
Kauli hiyo ilimuibua Ole Sendeka, ambaye aliomba mwongozo wa Spika kwa mujibu wa kifungu cha 76 na 71 (9).
Ole Sendeka alisema: “Taarifa ya Mwigulu akitoa majibu kwa Matiko alieleza malipo aliyofanya lazima apate idhini ya Rais na baadae aweze kulipa . Kwa mujibu wa katiba ibara ya 35 shughuli zote za serikali ya Jamhuri ya Muungao wa Tanzania zitatekelezwa na watumishi kwa niaba ya Rais.
“Taratibu za masharti ya kutoa fedha za serikali hata za mfuko mkuu wa hazina zinabainishwa katika ibara 36, 137 na 40 anayeweza kuidhinisha fedha ni Rais au Waziri aliyemteua.
“Sasa tunaposema malipo haya yanapaswa au kupitiwa na Rais, ili hali Rais mwenyewe juzi amesimama na kutoa malalamiko yake ya kutoridhishwa baadhi ya wakandarasi wanavyocheleweshewa malipo yao na kusababisha riba zaidi ya bilioni 400.
“Sasa najiuliza Rais kama ndio angekua ameidhinisha malipo haya na sio wale aliowakasimu mamlaka kwa aliowateua, kwa maelezo ya Waziri maana yake yote yanaidhini ya Rais jambo ambalo si kweli hata kidogo.
“Pengine ufisadi huu usingekuwa tunawataka maafisa masuuli na mlipaji mkuu wa serikali ambaye tunamsimamia na Waziri mwenye dhamana ya fedha, je ni sahihi kutumika kwa jina la Rais katika mazingira hayo kama kanuni ya 71 (9) inavyoeleza, naona jambo hili si jema linalopeleka taswira ya Rais kwamba lazima aidhinishe fedha katika kipindi hiki, ambacho wimbi la ufisadi limeweza kubainishwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Serikali.
“Naomba mwongozo wako ni sahihi kutumia maneno aliyotumia Waziri wakati wabunge wanaeleza masikitiko ya baadhi ya malipo ambayo hayajakaa vizuri?
Akitoa ufafanuzi, Spika wa Bunge Tulia Acksoni alisema: “Wakati akitoa taarifa Mheshimiwa Mwigulu alieleza kuwa sehemu pesa hiyo haijalipwa hata hivyo hayo madai Rais ameyafahamu kwa sababu amepelekewa, kwa muktadha wa Mwigulu hiyo taarifa aliyoitoa mheshimiwa Rais hakuna malipo yoyote yanayofanyika bila yeye kufahamu hata hili lilifika kwake kwa sababu madai yanayodaiwa lazima yeye aidhinishe.
“Hoja hapa ni Yeye (Rais) ndie anayeidhinisha. Mwongozo uliyeombwa ni hivi Je Rais ndiye anayeidhinisha malipo kama ambavyo ulitoa maelezo, yapi anayohusika na yapi hahusiki ili kumtenga Rais na haya ambayo yanatokea kuna mahali fedha zimelipwa bila utaratibu au kuna mahali fedha zimeliwa, maana kama zimeliwa na yeye ndio anaidhinisha maana yake anafahamu kuwa zimeenda kuliwa.
Jina la Rais lisitumike kwa namna hiyo kwa mujibu wa kanuni za bunge”.
Akijibu Mwigulu amesema: “Ipo namna hii kuna mlipaji mkuu wa serikali ambaye ni Katibu Mkuu wa Wizara ya fedha, lakini ili ifike kwenye ulipaji Katibu Mkuu haamki tu akapokea nani za wizara za kisekta halafu akalipa, kwa hiyo kuna utaratibu wa kuidhinisha matumizi.
“Sasa matumizi ni (bracket) kubwa kama tunavyoleta bajeti hapa hatuleti tu hapa (tax merges) hatua za ulipaji kuna malalamiko hili limechelewa …. idhini upata tarehe 17 ya kila mwezi.
“Jambo hili ni kubwa na la kisheria lazima tupate idhini ya mwanasheria mkuu na jambo kubwa, hivyo lazima tumuhusishe mwenye nchi, kuna wizara ambazo ufanyaji kazi wake, mfano Tamisemi mwenye wizara ni Rais, Wizara ya Fedha hatuwezi kufanya malipo bila kumpa taarifa Rais kwamba tumepokea invoice …tangu nipo Naibu Waziri utaratibu mkishafanya ‘celling’ katika mwezi ifikapo tarehe 10 ya kila mwezi lazima iwe imefika ofisini mwa Rais.
“Awamu ya nne, ya tano na hii ipo hivyo, na hiyo ‘celling’ ikishapata ‘go ahead’ ndio inaenda kwa Katibu Mkuu kwa ajili ya malipo.”
Spika Tulia : Neno Rais anayeidhinisha malipo ni sahihi au sio sahihi?
Mwigulu: Ni katika ‘levels, ‘celling’ lazima ipate idhini kwa Rais.
Tulia: Waheshimiwa wabunge nimeombwa muongozo hapa, lakini ile kanuni aliyeitumia Ole Sendeka ya 71 (1G) inazungumzia bila kuathiri masharti ya katiba ya kifungu cha 100 yanayolinda na kuhifadhi uhuru wa mawazo katika bunge, mbunge hatotumia jina la Rais kwa dhihaka au kulishawishi bunge kuamua jambo lolote kwa namna fulani.
“Ametupeleka pia vifungu kadhaa kwa katiba ibara 136,137 malipo kutoka mfuko mkuu wa serikali na ibara ya 35 (1) inayoeleza utekelezaji wa shughuli za serikali na namna Rais anavyokasimu madaraka yake, inasema shguhuli zote za utendaji wa serikali zitatekelezwa na watumishi wa serikali kwa niaba ya Rais.
“Kipengele (2) Amri na maagizo mengine yanayotolewa kwa madhumuni ya ibara hii yatadhibitishwa kwa namna itakavyoelezwa katika kanuni zilizowekwa na Rais kwa kuzingatia masharti ya katiba hii.
“Sehemu ya msisitizo ni yatadhibitishwa kwa namna katika kanuni zilizowekwa na Rais, kwa hiyo shughuli za serikali zinavyofanywa na waliokasimu ni wasaidizi wake.
“Namna muheshimiwa (Mwigulu) alivyoeleza yale malipo kwamba Rais anaidhinisha kwa mwongozo wa katiba yetu, malipo hayo yanafanywa na maafisa waliokasimishwa na sio Rais, kwa hiyo lile neno idhini kuwa Rais ndio anaidhinisha malipo katiba yetu imeshawekwa wazi.
“Sasa kwa mwongozo uliomba Sendeka jina la muheshimiwa Rais kwa maana ya matumizi mtoa taarifa hakutumia jina la Rais kwa dhihaka, hilo limeondoka.
“Lakini kwa Rais kupata taarifa kuna jambo fulani, kuna malipo fulani si kwa kutaka idhini kwa Rais alishakasimu, Rais hahusiki kwenye jambo hili la malipo moja kwa moja, kwa hiyo pia hahusiki kuwa amefanya malipo halafu ukaguzi umefanyika tunaanza kunyoosha mikono.”