Wabunge wacharuka suala la ushoga

WABUNGE wamecharuka kuhusu suala la ushoga nchini na kutaka serikali ichukue hatua za haraka kukabiliana nalo kama ambavyo inakabiliana na magonjwa ya mlipuko.

Wabunge hao Janeth Masaburi, Kunti Majala, Katani Ahmed na Joseph Kasheku ‘Musukuma’ walicharuka na kudai kuwa hata bungeni na baadhi ya viongozi wanajihusisha na matendo hayo.

Akichangia hotuba ya ofisi ya Waziri Mkuu, Mbunge wa kuteuliwa Janeth Masaburi amesema wazazi wameacha kulea Watoto wao na matokeo yake Watoto wamekuwa wakilelewa na majirani na wengine kujilea wenyewe huku wazazi wakiwa ‘busy’ kutafuta pesa.

Advertisement

Akirejea maandiko ya kwenye biblia katika kitabu cha mwanzo kuhusu kisa cha sodoma na gomora, Masaburi alidai kuwa wanaotetea ndoa na mahusiano ya jinsia moja ni  mke wa Lutu wa kwenye biblia ambaye aligeuka jiwe la chumvi.

“Kuna watu wengi ni wake wa Lutu humu, wanatetea ushoga, aliposhoga kuna basha, mashoga wanaonekana kwa urahisi, mabasha wapo wapi?  …mabasha hawawezi kutambulika na ndio wenye pesa…wahasiwe…kabla hawajahasiwa wachapwe viboko hadharani kama tulivyoona kwa Wahindi….Uganda na Wamasai waliomchapa yule mtu aliyewasaliti.

“Tumeongelea miradi mingi, matrilioni ya pesa, tuna Madini, Maziwa, Bahari rasilimali nyingi lakini tuwekeze kwa Watoto waadilifu, haya majizi, mafisadi tunayoyaona yanatokana na malezi, ukimtengeneza mtoto ataiga vitu vizuri, usipomtengeneza ataiga vitu vibaya, China, Singapore wamewekeza  kwenye watoto.

Nae Mbunge wa Kibamba Issa Jumanne Mtevu akiomba taarifa  amesema “kwenye eneo la maadili si tu wazazi nyumbani, si tu serikali kutengeneza mfumo,  inasemekana hata ndani ya bunge hili inasemekana, sina uhakika inasemekana wapo.

Mwenyekiti wa Bunge Daniel Sillo, alimuhoji Mbunge Masaburi kama amepokea taarifa nae alijibu amepokea.

“Taarifa naipokea, wengine ni viongozi tunawajua..waache.. tunamuongopa Mungu tu na si wanadamu…sisi wanadamu si kitu tupo duniani lakini kizazi lazima tukiendeleze.”Amesema

Kwa upande wa Mbunge wa Tandahimba Katani Ahmed akichangia hoja amesema wabunge ni kioo cha jamii na kumshauri Waziri wa Afya Ummy Mwalimu kupeleka wataalamu bungeni ili wabunge wote waweze kupimwa.

“Mheshimiwa Mwenyekiti (Daniel Sillo) kukiwa na magonjwa ya mlipuko kama Covid, Ebola tunaona serikali inakimbilia kufunga mipaka na kuwekeza nguvu kubwa kukabiliana na mlipuko, hili suala la ushoga kwa sasa hivi ni janga.

“Wabunge ni kioo cha jamii kabla hatujatoka huko nje kupaza sauti kwa wananchi wetu tunatakiwa kuanza na sisi kwanza, Mhe Ummy (Waziri wa Afya), tuletee wataalamu humu wakae pale mlangoni hakuna kuingia bungeni mpaka uwe umepimwa, iwe kama kipindi cha Covid 19 kila mtu lazima achanjwe hakuna kusafiri mpaka uchanjwe na humu bungeni hiyo hivyo hivyo.

Akiomba taarifa Mbunge wa Viti Maalum Kunti Majala alisema “Madaktari waletwe jumatatu humu wabunge wote tupimwe, ili tuweze kutoka mbele ya jamii na kupaza sauti kukemea ushoga

Kwa upande wa Msukuma alisema “hili bunge lipo ‘live’  tukizungumzia ufisadi watu wanasikiliza, tukizungumzia ushoga mnafanya masihara, mnataka lifanyike kimya kimya, magonjwa ya mlipuko serikali inachukua hatua haraka kwa nini ili kuna ugumu?” alihoji