Wabunge waijia juu FCC uuzaji Tanga Cement

WABUNGE wengi wamepinga Kiwanda cha Saruji cha Twiga kununua hisa za Kiwanda cha Saruji cha Tanga.

Walisema hayo wakati wanachangia hotuba ya makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Mbunge wa Mkinga, Dastan Kitandula alisema wananchi wa Tanga alisema hawataki kuona Tanga Cement inataifishwa.

“Hii ndiyo hofu yetu wakazi wa Tanga. Tunachohitaji utaratibu ufanyike,” alisema Kitandula.

Mbunge wa Misungwe, Alexander Mnyeti (CCM), aliishauri serikali ilinde wawekezaji wa ndani na kama serikali ikiruhusu kiwanda cha saruji cha Twiga kununua hisa za kiwanda cha Tanga itaondoa ushindani na watu wachache watatawala bei za bidhaa hiyo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Tauhida Nyimbo (CCM) amemshauri Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara kuliangalia kwa makini jambo hilo ili lifanywe kisheria.

Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa aliishauri serikali izingatie taratibu za kisheria katika suala la mauziano ya hisa.

Mbunge wa Bunda Vijijini, Mwita Getere alisema Kiwanda cha Saruji Tanga ni mali ya wananchi, hakitakiwi kuuzwa wala kubinafsishwa.

Mbunge wa Gairo (CCM), Ahmed Shabiby alisema: “Tunachotakiwa kukifanya ni kuhakikisha je, kiwanda kitafanya kazi baada ya kuuzwa?

Wafanyakazi hawatapoteza ajira zao?

Wabunge pia waliishauri serikali ihakikishe viwanda vyote vilivyobinafsishwa na havifanyi kazi vinarejeshwa serikalini ili wapewe watu wengine.

Mbunge wa kuteuliwa, Riziki Lulida alisema viwanda vingi ambavyo vimebinafsishwa havifanyi kazi na vimechangia kukosekana kwa ajira.

Habari Zifananazo

Back to top button