MKUU wa Mkoa wa Mtwara, Kanali Ahmed Abbas ameahirisha kikao cha kutathimini utekelezaji wa usambazaji wa umeme vijijini Mkoani Mtwara, baada ya wabunge kulalamikia utendaji hafifu wa wakandarasi ambao wanaotekeleza miradi hiyo kwenye majimbo yao.
Baada ya kuahirisha Kanali Abbas aliwataka Wakala wa Umeme Vijijini (REA) na wakandarasi kukaa na wabunge na kujadili maridhiano kuhusu malalamiko ya wabunge hao.
Kikao hicho ambacho kiliitishwa na Mkurungezi Mkuu wa REA nchini, Mhandisi Hassan Saidy kiliongozwa na Kanali Abbas.
Kikao hicho kilihusisha wakandarasi ambao wanatekeleza miradi ya REA Mkoani Mtwara, watendaji wa REA pamoja na wabunge.
Awali akizungumza katika kikao hicho, Mbunge wa Jimbo la Nanyumbu Yahya Mhata amesema kati ya vijiji 42, ambavyo vilipangwa kulinganishwa na umeme kwenye Mradi wa REA III, mzunguko wa kwanza ni kijiji kimoja kimeunganishwa.
Naye Mbunge wa Tandahimba, Katani Katani amesema mpaka sasa ni vijiji 13 Kati ya vijiji 83 vinaungashwa, huku zimebaki siku 20 tu muda wa utekelezaji wa mradi wa kuunganisha umeme kwenye vijiji hivyo kuisha
Akizungumza mara baada ya kuahirishwa kwa kikao hicho, Mhandisi Saidy amesema watakaa na wakandarasi pamoja na wabunge kama Mkuu wa mkoa alivyoagiza na kuangalia ni wapi penye shida ili kuchukua hatua za kisheria.