Wabunge waonya raia kubambikiwa kesi hifadhini

DODOMA; WABUNGE wamesema kumekuwa na malalamiko ya wananchi kukamatwa, kuteswa na kubambikiwa kesi na baadhi ya askari wa wanyamapori.

Akiwasilisha taarifa ya Kamati ya Ardhi, Maliasili na Utalii kuhusu utekelezaji wa bajeti ya Wizara ya Maliasili na Utalii mwaka wa fedha 2023/24, pamoja na maoni ya Kamati kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo mwaka wa fedha 2024/25, Mwenyekiti wa kamati, Timotheo Mnzava, amesema matukio hayo yanaongeza uhasama baina ya wananchi na askari hao.

“Katika maeneo yanayopakana na hifadhi nchini kumekuwa na baadhi ya matukio ya migogoro baina ya askari wa hifadhi na wananchi.

“Migogoro hiyo imezaa uhasama ambao umesababisha matukio ya kushambuliana na kusababisha ulemavu na wakati mwingine vifo baina yao.

“Mheshimiwa Spika, pia kumekuwa na malalamiko ya wananchi kukamatwa, kuteswa na kubambikiwa kesi na baadhi ya askari wa uhifadhi hali inayoongeza uhasama baina yao.

“Mathalani, katika moja ya matukio ambayo mahakama imethibitisha mwananchi kubambikiwa kesi na askari wa uhifadhi, ni lile la mwananchi aitwae Richard Changei Ng’ombe mkazi wa Wilaya ya Serengeti, ambae alikamatwa siku ya tarehe 12 Agosti, 2022 majira ya saa 12:00 jioni  na askari watano.

“Mheshimiwa Spika, baada ya mtuhumiwa huyo kufikishwa mahakamani, mahakama ilipitia ushahidi wa vielelezo mbalimbali vilivyowasilishwa mahakamani ikiwa ni pamoja na point za dira (cordinates) na nyara ambazo walidai wamemkamata nazo mtuhumiwa.

“Ushahidi wa askari ulitofautiana na kuonesha mtuhumiwa alibambikiwa kesi hiyo,” amesema na kuongeza:

“Mheshimiwa Spika, Katika hukumu ya kesi hiyo ambayo ni ‘‘Criminal Appeal No. 40809 of 2023‘‘, iliyosomwa tarehe 24 Aprili, 2024, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Musoma, Mhe. Kamazima Idd Kafanabo, wakati anamuachia huru mtuhumiwa Richard Changei Ng’ombe alitoa onyo kwa kusema:

‘‘Mahakama haiwezi kufumbia macho jambo hili linaonekana kuzoeleka na kujirudia la kutofuata maadili ya kazi kunakofanywa na maofisa wengi wa uhifadhi na wengine katika haki jinai, hasa katika ukamataji wa watuhumiwa na uchukuaji wa vielelezo,” amesema akinukuu sehemu ya hukumu hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button