Wabunge wapongeza shirika la nyumba

MWENYEKITI wa Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Uwekezaji na Mitaji ya Umma, Jerry Silaa amelipongeza Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) kwa mipango yake mizuri pamoja na kuendelea na ujenzi wa miradi ya nyumba iliyosimama.

Pamoja na pongezi hizo pia aliagiza (NHC) kuendelea na kasi ya ukusanyaji madeni yanayofikia Sh bilioni 26 kwa wadaiwa sugu.

“Shirika limeendelea na ujenzi wa nyumba kwenye miradi iliyokuwa imesimama kama Kawe na Morocco ambayo Watanzania wamekuwa wakipita na kuiona kuwa miradi imekaa muda mrefu,” alisema.

Kuhusu madeni sugu, Kamati ilisema hadi Desemba mwaka jana, NHC inadai Sh bilioni 26 kwa wadaiwa sugu.

Mwenyekiti wa Kamati hiyo alisema kwamba wameagiza kasi ya kudai madai hayo iongezwe.

Aidha, alipongeza NHC kwa kutekeleza kwa asilimia 100 maagizo yaliyotolewa na kamati hiyo mwaka jana.

Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa NHC, Dk Sophia Kongela alisema maelekezo ya nyuma yaliyotolewa na kamati yalikuwa ni pamoja na kujenga nyumba kwa gharama nafuu na kuhakikisha kuwa kodi inakusanywa, jambo ambalo limeendelea kutekelezwa.

Naye Mkurugenzi wa NHC, Nehemia Mchechu alisema shirika hilo limejipanga kuhakikisha madeni yanakusanywa na kutoa mikopo yenye riba nafuu kwa ajili ya nyumba za Watanzania.

 

 

Habari Zifananazo

Back to top button