Wabunge wapongeza ufaulu Lindi Sekondari

Wabunge wapongeza ufaulu Lindi Sekondari

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC), imeipongeza Shule ya Lindi Sekondari kwa maendeleo makubwa kwenye ufaulu wa wanafunzi hasa kidato cha sita.

Pongezi hizo wamezitoa leo Alhamisi walipoitembelea shule hiyo kwa ajili ya ukaguzi wa fedha zilizotolewa na serikali kwa lengo la ukarabati na ujenzi wa madarasa mapya.

Akitoa pongezi hizo, Mwenyekiti wa Kamati hiyo, Halima Mdee, amesema anaipongeza shule na walimu wote kwa kuutoa Mkoa wa Lindi kutoka mikoa ambayo ilikuwa haiheshimiki kwenye maendeleo ya elimu hapa nchini.

Advertisement

Amesena mabadiliko hayo makubwa ya elimu, mikakati iliyowekwa iendelezwe na kuendelea kuwapa  nguvu zaidi walimu, ili wajitume zaidi.

Awali akisoma taarifa, Mkuu wa Shule, Mwalimu Ramadhani Divelle, amesema Shule ya Lindi Sekondari kwa kidato cha sita ndani ya miaka mitatu mfululizo hali ya taaluma kwa kipindi hicho  imefanya vizuri sana.

Amesema matokeo ya kidato cha sita mwaka 2020, shule ilikuwa na watahiniwa 204 kati ya hao watahiniwa 27 walifaulu kwa daraja la kwanza, watahiniwa 130 walifaulu kwa daraja la Pili, watahiniwa 44 walifaulu kwa daraja la tatu na watahiniwa 3 walifaulu kwa daraja la nne, ufaulu huo ukiwa ni asilimia 100.

Amesema mwaka 2021 watahiniwa walikuwa 173 na kati ya hao 93 walifaulu kwa daraja la kwanza, 53 daraja la Pili, 27 daraja la tatu, ikiwa ni ufaulu wa asilimia 100.

“Mwaka 2022 Shule ilikuwa na watahiniwa 232 na Kati ya hao 116 walifaulu kwa daraja la kwanza, 105 walifaulu kwa daraja la Pili na 11 walifaulu kwa daraja la tatu, ikiwa ni ufaulu wa asilimia 100,” amesema.