Wabunge waridhishwa ujenzi mabweni VETA

KAMATI ya Kudumu  ya Bunge ya Hesabu za Serikali (PAC), imeridhishwa na matumizi ya fedha kwenye  ujenzi wa mradi wa mabweni mawili ya walimu tarajali Chuo cha Ualimu wa Ufundi Stadi Morogoro  (MVTTC) ,yaliyogharimu zaidi ya Sh bilioni 1.087.

Makamu Mwenyekiti wa kamati hiyo, Japhet Hasunga alisema hayo kwa niaba ya wabunge ambao ni wajumbe wa kamati hiyo, baada ya kufanya ukaguzi  wa ujenzi wa mabweni hayo Machi 19,2023, mjini Morogoro ambayo yana uwezo wa kuchukua walimu tarajali 96.

“ Kamati imeridhishwa na thamani ya fedha iliyotumika katika ujenzi wa mabweni hawa mawili , tunaipongeza  Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA)  kwa kazi nzuri walioifanya,” alisema Hasunga.

Kamati hiyo ya Bunge imeutaka uongozi wa mamlaka hiyo kutengeneza na kuweka samani katika mabweni hayo, ili yaanze kutumika na wanafunzi haraka iwezekanavyo.

Naye Mjumbe wa  kamati hiyo, Mhandisi Isaac Kamwelwe, amesema ujenzi wa mabweni hayo umezingatia hatua zote muhimu za majenzi na kuwataka  wakandarasi wazawa wanaopewa zabuni, wajenge majengo yenye kulingana na viwango vinavyokubalika .

Naye Naibu Waziri wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Omary Kipanga aliihakikishia  kamati hiyo ya kwamba wizara itatekeleza maagizo yote yaliyotolewa ya kutengeneza samani za mabweni katika kipindi kifupi kijacho.

“ Sisi wizara tunarudi kujipanga kuhakikisha ifikapo Aprili mwaka huu tunapata Sh  milioni 54 na kukamilisha samani zote zinazohitajika katika mabweni haya, ili vijana wanapokuwa wanafungua chuo muhula ujao waweze kutumia, “  alisema Naibu Waziri Kipanga.

Kwa upande wake Katibu Mkuu Wizara  hiyo, Profesa  Carolyne Nombo  alisema  ujenzi wa mabweni hayo umegharimu  Sh bilioni 1.087 na kwamba  wizara na mamlaka husika zipo tayari kuyatunza kwa ajili ya matumizi ya sasa na vizazi vijavyo.

Awali Kaimu Mkurugenzi VETA ,  Anthony Kasore  akitoa taarifa mbele  ya kamati hiyo, alisema  kuwa Benki ya Maendeleo ya Afrika (AfDB), ilitoa mkopo wa Sh bilioni 1.214,  ambapo mkataba wa utekelezaji ulisainiwa Agosti 29, 2018.

Habari Zifananazo

Back to top button