Wabunge wataka sekta binafsi uendeshaji wa Bandari Dar

WABUNGE wametaka Bandari ya Dar es Salaam iboreshwe zaidi ikiwa ni pamoja na kuruhusu sekta binafsi kuingia mkataba ili kuendesha shughuli za bandari hiyo.

Walisema hayo bungeni Dodoma jana wakati wakichangia kwenye mjadala wa makadirio ya mapato na matumizi ya Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi kwa mwaka wa fedha 2023/2024.

Katika bajeti ya wizara hiyo, Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa ameomba kuidhinishiwa Sh 3,554,783,957,000.

Kati ya fedha hizo, Sh 1,468,238,449,000 ni kwa ajili ya sekta ya ujenzi na Sh 2,086,545,508,000 ni kwa ajili ya sekta ya uchukuzi.

Mbunge wa Viti Maalumu, Catherine Magige (CCM) alisema Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari (TPA) kwa mujibu wa sheria namba 7 ya mwaka 2019 inapaswa kuruhusu ushirikishwaji wa sekta binafsi kimkataba.

“Serikali iingie mkataba na kampuni yenye uwezo ili kuepuka ucheleweshaji bidhaa bandarini na kuwapa hasara wafanyabiashara na pia itaongeza tija na mapato kwa serikali.”

Alisema Bandari ya Dar es Salaam ina changamoto nyingi ikiwamo mifumo ya Tehama, haina viwango vya tija kwa bandari, idadi ndogo ya miundombinu kuendesha bandari na imefikia ukomo kuhudumia shehena kubwa ya mizigo.

“Wafanyabiashara wanasubiri kutoa makontena wiki tatu hadi miezi miwili mitaji yao inakata, bidhaa zinapanda, imekuwa shida. Inasemekana kutoa mzigo Korea hadi Dubai unatumia Dola za Marekani 500 lakini Dubai hadi hapa ambapo ni karibu unatumia Dola 4,000, tubadilike,” alisema.

Mbunge wa Kibiti, Twaha Mpembenwe (CCM) aliitaka serikali kuja na mpango mkakati wa kuboresha uendeshaji wa bandari ili kuongeza mapato.

“Mkurugenzi mtendaji na wasaidizi wake wanafanya kazi vizuri tuwape moyo, tusikae na mawazo ya kizamani nchi itauzwa. Bandari ichangie pato la taifa, bandari inatengeneza fedha za kutosha… life expectance ya Singapore ni miaka 85 lakini Tanzania miaka 61 kwa sababu uchumi wetu si endelevu. Njooni na mpango mkakati tuboreshe bandari yetu,” alisema Mpembenwe.

Mbunge wa Kigoma Mjini, Kilumbe Ng’enda (CCM) alisema hii ni bajeti ya mwisho ya wizara hiyo kuiunga mkono hadi atakapoona meli imeshushwa kwenye Ziwa Tanganyika. Alisema sasa hakuna meli hata moja inayotoa huduma kwenye ziwa hilo.

Mbunge Singida Mashariki, Miraji Mtaturu (CCM) alitaka TPA itumike vizuri ili ilete mchango zaidi kwa serikali.

Habari Zifananazo

Back to top button