WABUNGE wameishauri serikali iweke utaratibu mzuri inapopitisha benki fedha za mikopo kwa wanawake, vijana na wenye ulemavu.
Walisema hayo bungeni Dodoma jana wakati wanachangia makadirio ya mapato na matumizi ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi).
Mbunge wa Viti Maalumu, Zainab Katimba (CCM) alisema kwa kuwa serikali imeamua fedha za asilimia 10 za vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia benki, Tamisemi ihakikishe gharama za usimamizi wa fedha hizo zisitokane na mfuko huo.
Pia alishauri wanufaika wa mikopo hiyo wajengewe uwezo kwa kuundiwa programu za mafunzo kuhusu matumizi ya fedha hizo.
Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo (CCM), alisema katika Jiji la Arusha kuna changamoto katika usimamizi wa fedha za halmashauri.
Gambo alidai kuwa kuna ujenzi wa jengo la utawala unaoendelea la ghorofa zaidi ya sita lakini alitafutwa fundi mjenzi bila kutangaza zabuni, taratibu za manunuzi hazikufuatwa bali alitafutwa tu mtu wakasaini naye mkataba na kumpa kazi kwa gharama ya Sh milioni 199.7.
“Pia wamenunua vifaa vya shilingi milioni 132 ambavyo havijathibitika kufika eneo la ujenzi, wameongeza nondo tani 6.48 zenye thamani ya shilingi milioni 17, pia kumekuwa na malipo feki kwa kuwa na risiti feki za EFD za kiasi cha Sh milioni 699.9,” alisema Gambo.
Mbunge wa Viti Maalumu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Halima Mdee alishauri Tamisemi imuagize Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) afanye ukaguzi wa kiuchunguzi ili kubaini waliohusika na ubadhirifu mikopo ya asilimia 10 kwa wanawake, vijana na watu wenye ulemavu.
Mdee alidai kuwa katika taarifa za CAG ikiwemo ya mwaka jana ilifanya majumuisho ya fedha ambazo hazijarudishwa kwa kipindi cha miaka mitano kwenye mfuko wa vijana, wanawake na watu wenye ulemavu.
Mdee alidai kuwa mwaka jana fedha ambazo hazikurejeshwa zilikuwa Sh bilioni 47.1 na za miaka mingine minne ya nyuma yake zilikuwa zaidi ya Sh bilioni 100 ambapo zikijumlishwa na fedha za mwaka huu ambazo ni Sh bilioni 88, zinakuwa zaidi ya Sh bilioni 188.
Alisema pamoja na maelekezo mahususi 14 ya Waziri wa Tamisemi, Angellah Kairuki, kwa Mamlaka za Mikoa na Halmashauri hakuna mahali ambapo Waziri ametoa maelekezo kwa wakuu wa mikoa na wakurugenzi wa halmashauri kuhakikisha fedha hizo zilizopotea katika maeneo yao ziweze kupatikana.
“Lazima watu wawajibike, Rais anahangaika, fedha zinakuja halafu watu wachache huku chini wanapiga (wanaiba), serikali ifanye ukaguzi wa kiuchunguzi ili kujua kama kuna udanganyifu, ubadhirifu au rushwa,” alisema Mdee.