Wabunge wataka uwekezaji kilimo cha umwagiliaji

WABUNGE wameishauri serikali iongeze uwekezaji kwenye kilimo cha umwagiliaji ili kuleta mageuzi ya sekta hiyo.

Pia, wameihimiza serikali iitazame upya Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB) kwa kuipa nguvu ikopeshe wakulima wakiwamo wa kawaida ifike hadi vijijini.

Wameyasema hayo bungeni Dodoma wakati wanachangia makadirio ya mapato na matumizi ya fedha ya Wizara ya Kilimo kwa mwaka huo wa fedha 2023/2024.

Mbunge wa Musoma Vijijini, Profesa Sospeter Muhongo (CCM) alisema tafiti zinaonesha kilimo cha umwagiliaji kina tija zaidi kuliko cha kutegemea mvua.

“Kwa mfano, mahindi yakilimwa katika eneo la eka moja na kutegemea mvua, mkulima anaweza kuvuna tani moja hadi tatu za mahindi, lakini mahindi hayo hayo yakilimwa kwenye eka moja inayotegemea umwagiliaji anaweza kuvuna tani tano hadi saba,” alisema Profesa Muhongo.

Alisema ni muhimu kuwekeza katika kilimo kinachotumia trekta na kuwekeza kuzalisha mbegu bora, akisema nchi nyingi zinatumia kilimo kama biashara. Alitoa mfano wa China inayoongoza kuuza mchele duniani na Marekani na India zinauza mahindi.

“Wizara iangalie fursa hizi za biashara na sisi tuzalishe mahindi, mchele, ngano na mazao mengine. Tunaweza kuzalisha mahindi na kushindana na Nigeria katika soko la Afrika,” alisema Profesa Muhongo.

Mbunge wa Mbarali, Francis Mtega (CCM) alisema kilimo cha umwagiliaji ni jibu la changamoto za mabadiliko ya tabianchi na ni ukombozi kwa wakulima.

Mbunge wa Viti Maalumu, Anatropia Theonest (Chadema) alisema taarifa zinaonesha kilimo kimeshuka na kikishuka ni ina maana umasikini unazidi kwa wananchi.

Mbunge wa Magu, Kiswaga Destery (CCM), alisema ni muhimu mapinduzi ya kilimo yaendane na hali halisi ya tabianchi na akaipongeza Wizara ya Kilimo kwa kuja na mikakati ya umwagiliaji.

Destery aliishauri serikali itafute mbinu mbadala kupunguza ununuzi wa mazao kama vile ngano kutoka nje ya nchi.

“Tunatumia hela nyingi sana kununua ngano. Njombe na Katavi tunaweza kulima ngano. Tutaagiza mpaka lini kwanini tusiwe na mkakati mahsusi wa kulima ngano ili tuachane na kuagiza nje? Alihoji.

Mbunge wa Kwela, Deus Sangu (CCM) alimpongeza Rais Samia Suluhu kwa kutoa ruzuku kwenye mboleo jambo ambalo limewasaidia na kuwainua wakulima.

Mbunge wa Bahi, Kenneth Nollo (CCM), alisema ni muhimu kuwekeza zaidi katika kilimo cha umwagiliaji kwa kuwa kwa sasa pamoja na kuwepo na eneo kubwa la ardhi ya umwagiliaji bado ni eneo dogo ndio linalotumika.

Habari Zifananazo

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button
0
Would love your thoughts, please comment.x
()
x