Wabunge wataka uwiano wa kimkoa, kiwilaya nafasi za ajira
WABUNGE wameishauri serikali kupitia Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) izingatie uwiano wa kimikoa na kiwilaya inapotangaza nafasi za ajira.
Walisema hayo bungeni Dodoma jana wakati wakichangia makadirio ya mapato na matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2023/24.
Mbunge wa Madaba mkoani Ruvuma, Dk Joseph Mhagama (CCM) amesema ni muhimu serikali izingatie uwiano wa kimikoa na wilaya inapotangaza nafasi za ajira zikiwemo za walimu na watumishi wa afya ili kutoa fursa sawa kwa Watanzania wote.
Dk Mhagama alisema programu ya mafunzo kilimo biashara kwa vijana (BBT) imezingatia uwiano wa maeneo na pia hata ajira za majeshi huzingatia uwiano wa kimikoa.
Mbunge wa Mbulu Vijijini, Flatei Massay (CCM) alisema ajira mpya zinawatesa kwenye majimbo hivyo akaiomba serikali izingatie uwiano katika kuzigawanya kwa kuzingatia majimbo na halmashauri.
“Watendaji wa kata wanaajiriwa kutoka serikali kuu, rudisheni kwenye halmashauri ajira hizi ili ziweze kufanyiwa kazi wilayani. Mheshimiwa Spika halmashauri inaweza kupata nafasi 20 za kuajiri lakini utashangaa wanaokwenda kuajiriwa unaweza kukuta hata mtu mmoja hatokei kwenye eneo hilo kwenye ajira hizo 20, niiombe serikali, mnapoajiri hawa walimu, mjiridhishe kama kweli majina mnayoletewa yanatoka kwenye maeneo yetu,” alisema Massay.
Katika mjadala huo, Mbunge wa Viti Maalumu (CCM) kutoka Mkoa wa Tanga, Husna Sekiboko alisema moja la eneo litakalosaidia kuboresha elimu nchini ni kuhakikisha kila mtoto anapata fursa ya kusoma au kujifunza katika mazingira yanayostahili.
Sekiboko alisema pamoja na serikali kutoa elimu bure, bado kuna wazazi wanatumia gharama kati ya Sh 600,000 hadi Sh 1,000,000 kwa mwaka kuwapeleka watoto wao katika shule za kata kutokana na umbali zilipo shule, hivyo wazazi hulazimika kuwapangishia vyumba na kuwanunulia mahitaji mengine watoto wao.
Alisema elimu bila malipo wanaonufaika ni wale wanoishi karibu na hizo shule lakini wanaoishi mbali na shule hizo, wazazi hulazimika kuingia gharama kubwa.
“Tunapozungumzia suala la ujenzi wa mabweni tunaomba mlichukulie kama ni jambo maalumu linalohitaji jicho la tatu la serikali, hali ni mbaya, hatutaweza kupandisha kiwango cha elimu kwa kuweka kiashiria cha ufanisi wa utendaji (KPI), mwalimu ameshaandaliwa chuoni, ana uwezo wa kumfundisha afaulu kwa mujibu wa taaluma yake, ukimpelekea mpango nje ya taaluma yake unamfanya aache kufundisha na kuanza kushughulika na mpango ambao umepelekwa na Tamisemi,” alisema Sekiboko.
Mbunge wa Ukonga, Jerry Silaa alimwomba Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson awaelimishe wananchi wa jimbo lake kuhusu kazi za mbunge kwa kuwa wakati mwingine anapowatakia salamu za Pasaka au Iddi kwenye mitandao wao humweleza aachane na mambo hayo awajengee barabara.