Wabunge wataka waajiriwa wapya wabanwe wasihame

WABUNGE wameipa angalizo Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi) juu ya mgawanyo wa watumishi wapya elimu na afya kwamba izingatie maeneo yenye upungufu mkubwa na iwabane wasihame baada ya ajira.

Miongoni mwa wabunge waliochangia makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 yaliyowasilishwa juzi bungeni na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Angellah Kairuki walisema kumekuwa na mgawanyo usiozingatia usawa.

Wabunge wengine walisema kumekuwapo na tabia ya baadhi ya waajiriwa wapya kuripoti kwenye vituo na kisha kuhamishwa kwenda maeneo mengine wanayotaka na kufanya maeneo husika yaendelee kuwa na upungufu wa watumishi.

Mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby (CCM) alisema katika mgawo wa watumishi, majimbo ya mawaziri yamekuwa yakipata watumishi wengi tofauti na wabunge wengine wasio mawaziri.

Kwa upande wake, Mbunge wa Mlalo, Rashid Shangazi (CCM) alisema baadhi ya watumishi waliopangiwa jimboni humo, walihama kwa madai ya kuogopa baridi jimboni humo.

Mbunge wa Viti Maalumu, Hawa Mchafu (CCM) alizungumzia upungufu wa watumishi katika sekta ya afya na kutaka serikali ichukue hatua.

Angalizo la wabunge limetolewa wakati serikali ikiwa imetangaza ajira 21,000 kwa kada ya walimu na afya hivi karibuni.

Watakaoajiriwa katika kada za ualimu ni 13,130 watakaofundisha shule za msingi na sekondari. Kwa kada ya afya, wataajiriwa 8,070 watakaofanya katika hospitali za wilaya, vituo vya afya na zahanati.

Akisoma hotuba ya bajeti juzi, Angellah alisema hadi Februari, 2023 mahitaji ya walimu katika shule za msingi ni 362,189 kwa kutumia uwiano wa mwalimu mmoja kwa wanafunzi 45. Waliopo ni 175,864 na upungufu ni 186,325 sawa na asimilia 51.44 ya mahitaji.

Aidha, mahitaji ya walimu kwa shule za sekondari ni 174,632 na waliopo ni 84,700 na upungufu ni walimu 89,932 sawa na asilimia 51.5.

 

Habari Zifananazo

Back to top button