Wabunge wataka wezi fedha za umma wang’oke

Spika wa Bunge Dk Tulia Ackson

WABUNGE wamecharuka kuhusu wizi na ubadhirifu wa fedha za umma na wanataka wanaohusika wawajibike kwa kujiondoa kwenye nyadhifa zao.

Wamesema hayo bungeni Dodoma jana wakati wakichangia azimio la kumpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuimarisha demokrasia na kukuza diplomasia ya uchumi.

Walimpongeza Rais Samia mambo anayofanya likiwamo suala la maridhiano na kutaka Bunge lisaidie kuhakikisha yanayopitishwa yanasimamiwa na kutekelezwa.

Advertisement

Mbunge wa Ubungo, Profesa Kitila Mkumbo alimpongeza Rais Samia kwa kutekeleza kikamilifu ilani ya uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) na kusema katika siku 85 watakazokaa katika mkutano wa 11 wa bunge, wabunge wanataka kupata majibu serikalini kuhusu changamoto za kimfumo, kisheria na kikanuni kutoka kwa mawaziri.

“Mheshimiwa Rais kaongea kwa uchungu sana, sisi Tanzania hatuna utamaduni wa kupisha, kazi yetu wabunge tuoneshe wenzetu ambao Rais amewasema, tuoneshe mlango wa kutokea. Kazi hiyo duniani huwa haifanywi na serikali, huwa inafanywa na Bunge,” alisema Profesa Mkumbo na kuongeza:

“Tunatarajia Bunge hili, watu wote ambao Rais amesema wapishe, hawajaona mlango, sisi tuwaonyeshe mlango katika miezi hii mitatu. Hilo ni jukumu la msingi la bunge hili.”

Mbunge wa Simanjiro, Christopher Ole Sendeka (CCM) alisema waliopewa dhamana na Rais Samia baada ya tamko alilotoa wakati akipokea ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) na ripoti ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) wanapaswa kuwajibika.

“Hasira ya Mama Samia haiwezi kwenda bure.

Bunge lako tukufu lazima katika siku zinazokuja katika mkutano huu tutoe msimamo ambao utahakikisha kwamba hasira ya mama kwa wale wanaofisadi uchumi wa nchi hii wanachukuliwa hatua bila ya kutazama sura zao,” alisema Ole Sendeka na kuongeza:

“Tunataka wachukuliwe hatua, hatuwezi kumuunga mkono Rais kwa maneno, lazima tumuunge mkono kwa vitendo na kama hamtachukua hatua tukiwa kwenye Bunge hili tutakuja na hoja nyingine dhidi ya wale ambao wamekabidhiwa dhamana na Rais ya kuwashughulikia wale ambao bado hawajashughulikiwa.”

Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Msukuma (CCM) alihimiza wabunge wawe imara kuhakikisha wanaofanya ubadhirifu wa mali za umma hawasubiriwi kuondoka bali waondolewe.

“Hakuna mtu anayeweza kutoka kwenye mafuta kwa njia ya hiari…ngoma (sakata) hii ikija humu (bungeni), katika vituo ambavyo Spika Tulia (Dk Ackson) tutakukumbuka, hatutaki kupiga tena swaga… tunasubiri ngoma ije tulale nao mbele,” alisema Msukuma.

Akihitimisha mjadala, mtoa hoja, Mbunge wa Biharamulo Magharibi, Ezra Chiwelesa (CCM) alisema kazi anayoifanya Samia isipopata usimamizi wa bunge, itakuwa bure.

“Mazuri tuyalinde kwa kuhakikisha yote yanayopitishwa bungeni yanasimamiwa na kutekelezwa. Yaliyoombwa na wabunge muda ukiwadia kwa sababu ripoti ya CAG haijawasili humu, kiongozi (Spika) atajua namna ya kwenda nayo,” alisema Chiwelesa.

Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson alisema Rais anapofanya vizuri ni muhimu wabunge wamtie moyo.

Dk Tulia ametoa ufafanuzi kuwa ripoti ya CAG itakapopelekwa bungeni kwa mujibu wa katiba ndipo itakuwa wazi kwa umma.