Wachambuzi wataja faida Samia kuhutubia Bawacha

TANZANIA imetajwa kuwa katika nafasi nzuri ya kuimarika katika sekta za uwekezaji, biashara na utalii kutokana na maridhiano ya kisiasa yanayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.

Wachambuzi wa masuala ya siasa walilieleza HabariLEO jana kuwa matunda ya maridhiano yameanza kuonekana kutokana na kitendo cha Rais Samia kualikwa na kuhudhuria kongamano la Baraza la Wanawake wa chama hicho (BAWACHA) kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani.

Mtaalamu wa diplomasia na mchambuzi wa siasa nchini, Goodluck Ng’ingo alisema kitendo cha Rais Samia kuhudhuria kongamano hilo kinadhihirisha kuwa nchi ina amani, utulivu na maelewano.

Advertisement

“Miongoni mwa vitu vinavyovutia wawekezaji ni pamoja na sera za kudumu zisizobadilika pamoja na amani na utulivu wa kisiasa katika nchi.

“Kwa hali hiyo, ni dhahiri Tanzania inaenda kufaidika kama nchi kutokana na ongezeko la wawekezaji litakalotokana na utulivu na uhakika wa biashara,” aliongeza Ng’ingo.

Mchambuzi wa masuala ya siasa, Gabriel Mwang’onda alisema juhudi za Rais Samia za kujenga taifa lenye umoja, mshikamano na uzalendo zinajenga mazingira rafiki kwa biashara ya ndani na nje ya nchi hali itakayolifanya taifa kupata mapato zaidi.

Alisema kitendo cha Rais Samia kukubali kutengeneza taifa lisilo na mipasuko kinatuma ujumbe wa mshikamano na uzalendo.

Mhadhiri wa Chuo cha Diplomasia na mchambuzi wa masuala ya siasa, Deus Kibamba alisema Rais Samia ameonesha ni nguli wa siasa.

“Nampongeza Mheshimiwa Rais kutokana na utekelezaji wa mambo aliyoahidi tangu katika Mkutano wa Januari 3 (2023), alipokutana na viongozi wa vyama vya siasa na matunda yake ndio haya tunayoyaona sasa hivi,” aliongeza Kibamba.

Mhadhiri mstaafu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Mosha ambaye pia ni mchambuzi wa siasa nchini alisema mkutano wa Rais Samia na Baraza la Wanawake la Chadema ni mwanzo mzuri wa ujenzi wa Tanzania mpya.

Alisema siku zote uvumilivu wa kisiasa ambao Rais Samia ameuonesha unatakiwa kuigwa na viongozi wote wa vyama vya siasa ili kufanikisha kupatikana kwa Tanzania bora kwa kila mtu.

Mbunge wa Iringa Mjini, Jesca Msavatavangu alisema Rais ameonesha kuwa Chama Cha Mapinduzi (CCM) kinaenzi kwa vitendo suala la kujenga umoja wa kitaifa.

“Rais wa Watanzania wote bila kujali itikadi zao za kisiasa, imani zao za kidini, tofauti za makabila yao na rangi zao, tofauti za hali zao kiuchumi, Rais anawapenda Watanzania wote,” alisema Msavatavangu.