Wachangia Sh Mil 100 kusaidia watoto wenye saratani

Wachangia Sh Mil 100 kusaidia watoto wenye saratani

TAASISI ya Mo Dewji inayoshughulikia masuala ya  elimu, maendeleo ya jamii, afya na uwezeshaji wa kijinsia jana ilikabidhi hundi ya Sh milioni 100 kwa taasisi ya Tumaini la Maisha (TML), ambayo inashughulikia huduma kwa watoto wenye saratani Afrika Mashariki.

Kwa mujibu wa taasisi ya Mo Dewji, fedha hizo zilizokabidhiwa zinatokana na kuwapo kwa haja ya kuhakikisha watoto wenye saratani wanaotibiwa katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili wanapata huduma bora za afya, ambazo ni haki za binadamu.

Toka mwaka 2013, Mo Dewji  imekuwa ikishirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kupitia Tumaini la Maisha, Kituo Kikubwa zaidi cha Saratani ya Watoto Afrika Mashariki.

Advertisement

Taasisi hiyo ya Mo Dewji  mpaka sasa imechangia zaidi ya Sh bilioni moja kwa ajili ya kusaidia matibabu ya watoto wenye saratani nchini katika kipindi cha miaka tisa.

Mkurugenzi wa Mo Dewji Foundation, Rachel Carp akizungumza katika makabidhiano ya hundi hiyo ya Sh milioni 100 kwa Mwenyekiti wa Bodi wa Taasisi ya Tumaini la Maisha, Dk Gerald Mongella, alisema wataendelea kufanya kazi na Tumaini la Maisha kwa sababu programu zao ni muhimu sana kwa maisha ya maelfu kote Afrika Mashariki.

Alisema programu za taasisi hiyo zenye kutoa huduma za kiafya na zisizo za kiafya kwa watoto, kama vile ununuzi wa dawa za kemotherapia, usaidizi kwa programu ya shule, matengenezo ya mpango wa usafiri kwa wagonjwa na walezi wao, usaidizi wa programu ya tiba ya michezo kwa wagonjwa.

Programu nyingine ni usaidizi katika mafunzo ya stadi za maisha kwa wazazi, vifurushi kwa wagonjwa wapya waliolazwa, na usaidizi wa mshahara kwa wafanyikazi ambao sio wa afya zinahitaji mchango mkubwa ndio maana wamekuwa wakishirikiana nao.

Aliwahimiza Watanzania wote kuunga mkono juhudi muhimu za TLM na mashirika mengine yasiyo ya kiserikali yanayojishughulisha na kuwawezesha watu wengi wasiojiweza nchini Tanzania.

/* */