KAGERA; Bukoba. Wadau mbalimbali wa maendeleo mkoani Kagera wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera Fatuma Mwassa, wameshiriki harambee ya kuchangia ujenzi wa uzio wa hosteli ya wanafunzi wasichana katika Shule ya Bukoba Sekondari.
Harambee hiyo ilifanikisha kukusanya kiasi cha Sh Mil 51 fedha tasilimu, vifaa vya ujenzi na ahadi, ambapo kiasi cha Sh milioni 79 kinahitajika katika ujenzi wa uzio huo.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Mwassa amesema wadau ni chachu muhimu katika kukuza maendeleo, hivyo wakishirikiana na serikali wanaweza kuufanya mkoa wa Kagera kuwa kinara wa maendeleo na kujikwamua katika masuala ya kiuchumi.
Wadau wa maendeleo kutoka mtandao wa kijamii kupitia kundi la Whatsapp linalojulikana Kama Kagera mpya, wakiongozwa na muasisi wa kundi hilo Justine Kimodoi, alimpongeza Mkuu wa Mkoa kwa kuonesha njia.
“Tumejaribu sana kuanzisha vitu lakini hakuna lililofikia mwisho , kundi moja likianzisha lingine linapinga, serikali imekuwa ikianza vizuri na wadau, lakini baade kundi la watu wasio na nia njema wakijumuisha na siasa wanakuwa na nguvu sana miradi inaishia katikati , ” amesema kwa njia ya mtandao Kimodoi ambaye anaishi nje.
Karim Amri Mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), amesema ameona kwa mara ya kwanza kiongozi mkubwa aliyepambana na wadau wa maendeleo mpaka kutangaza ushind, huku akisema kuwa sasa ni zamu ya wilaya zote za Mkoa wa Kagera kuanza kufanya vizuri miradi yao kwa kushirikiana na wadau bila kumuacha mtu nyuma.
Kwa Niaba ya Mtandao wa WhatsApp aa Kagera mpya akitoa taarifa ya awali mwenendo wa michango tangu wazo lilivyotolewa Septemba mwaka huu, Jamali Karumuna ambaye aliwakilisha wadau wa maendeleo kama Mwenyekiti wao, amesema baada ya kukamilisha ujenzi wa uzio wa wanafunzi wa Bukoba Sekondari ,wadau watajenga uzio wa wanafunzi wa shule ya wasichana ya Omumwani Sekondari.
Comments are closed.