Wachangia Sh Mil 79 ujenzi wa bweni
KAGERA: Wadau wa maendeleo mkoani Kagera kwa kushirikiana na Mkuu wa Mkoa wa Kagera wamechangia kiasi cha Sh milioni 79.5 kwa ajili ya ujenzi wa bweni la wasichana wa shule ya Sekondari ya Omumwani ambalo liliteketea na moto Oktoba 22 mwaka huu na kusababisha mali za wanafunzi kuungua katika bweni hilo.
Wadau hao wameguswa na uchangiaji huo baada ya Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Fatma Mwassa kuandaa usiku wa pamoja maarufu kama “IJUKA OMUKA SOTE TUGUSWE GALLA DINNER”ambapo usiku huo ulitumika kujadili fursa za maendeleo zilizopo mkoani Kagera,hali ya uchumi na kuangazia mkoa ulikotoka na unakoelekea.
Licha ya wadau kupata usiku wa kufurahi na kushiriki hafla kwa pamoja na wakazi wanaoishi Mkoa wa Kagera na wale wa nje ya mkoa huo na kujadili namna ya kupata maendeleo mkoani hapo swala la uchangiaji wa bweni la wasichana lilioungua liliibuka katika hafla hiyo na kuanza mara moja huku wadau wa maendeleo wakisisitiza kuchangia bweni hakutoshi bali shule hiyo ijengewe uzio wa shule ili kuweka mazingira salama kwa watoto wa kike.
Mkuu wa Mkoa wa Kagera akatoa ombi kwa wadau waliohudhiria hafla hiyo.
“Ndugu wadau pamoja na kuwa tunapata usiku mzuri lakini mnamo Oktoba 22 shule ya wasichana ya Omumwani moja ya bweni la wasichana liliungua na kuleta huzuni kwa watoto wa kike,shule hiyo pia iko Nshambya karibu na makazi ya wananchi lakini hakuna uzio,kama kuna yeyote anaweza kuguswa tuchangie ili wanafunzi wakitoka likizo wapate sehemu nzuri ya kulala,naomba mniunge mkono mimi mama yenu katika kulifanikisha hilo,”alisema Mwassa.