WACHIMBAJI Wadogo wa madini Kanda ya Kati, wamekutana kwa siku mbili mkoani Singida, kuelimishwa na kukumbushana kuhusu masuala ya usalama, baruti na uhifadhi wa mazingira katika maeneo ya uchimbaji mdogo.
Mkurugenzi wa Huduma za Sheria Tume ya Madini, Dk. Anold Gasase, amesema tume hiyo imeandaa mkutano huo ili wataalam wake watoe mafunzo kuhusu shughuli za uchimbaji na uchenjuaji wa madini, kwa kuzingatia usalama, afya, taratibu na miongozo iliyopo.
“Umuhimu wa mafunzo haya unathibitishwa na vifo 139 vya wachimbaji wadogo wa madini na majeruhi 59 kwenye migodi tofauti nchini, kuanzia Mwaka 1918 na 2020,” amesema Dk. Gasase.
Amesema uchunguzi umebaini kiini cha ajali hizo ni wachimbaji kufukiwa na vifusi vinavyobomoka wanapokuwa mashimoni na kuwakosesha hewa.
Amesema shughuli hizo zina manufaa makubwa kwa wachimbaji na taifa kwa kutoa fursa za ajira, biashara na malipo ya kodi tofauti.
Dk.Gasase amewaomba washiriki wa mafunzo hayo, kujifunza, kuuliza maswali ili wafahamu mambo mbalimbali.
Mwenyekiti wa wachimbaji wadogo wa Mkoa wa Singida, Robert Malando, ametaja changamoto wanayokabiliana nayo kuwa ni umeme kukatika mara kwa mara, akaomba Tume hiyo na serikali kwa ujumla, kuwasaidia.
Mchimbaji wa madini katika Mgodi wa Mpipiti, Magdalena Lucas, amepongeza tume hiyo kwa kuwapa mafunzo hayo kwani yamewaongezea uelewa na utayari katika utekelezaji wa majukumu yao, ikiwemo kulipa kodi za serikali na mamlaka nyingine zilizo kwenye maeneo yao ya kazi.
Mafunzo hayo yanahitimishwa Leo, Januari 27 Mwaka huu.