Wachimbaji 8 wafa kwa kufukiwa na kifusi Geita

WATU nane ambao ni wachimbaji wadogo wamefariki dunia kwa kufukiwa na kifusi katika kijiji cha Igando, Kata ya Magenge wilayani Geita, wakati wakiendelea na shughuli za uchimbaji kwenye eneo lisilo rasmi.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Geita, Safia Jongo amethibitisha kutokea kwa ajali hiyo alipozungumuza na waandishi wa habari baada ya kuopoa miili eneo la tukio.

Kamanda Jongo amesema wachimbaji hao walikutwa na umauti huo majira ya saa tisa usiku, baada ya mvua kubwa kunyesha eneo jirani na maporomoko ya maji kuvamia mashimo walipokuwa wakichimba.

Kamanda amewataja waliofariki ni Juma Pamba (42), Akili Anthony (40), Samwel John (25), Juma Swalele (50), Simon Mabula (40) Kamala Nyambogo (30), Bahati Nyambogo (25), pamoja na Juma Sumuni (53).

“Tukio limetokea kijiji cha Igando, lakini marehemu karibia wote wanatokea Ipalamasa, huenda walikuwa hawajui hii marufuku ama walijua wakafanya kusudi na ndipo maafa kama haya yakawapata,” amesema.

 

Habari Zifananazo

Back to top button