Wachimbaji madini kuanzisha benki yao

WACHIMBAJI wa madini nchini wamekusanya zaidi ya Sh bilioni 2.8 kwa ajili ya kuanzisha benki yao itakayowawezesha kuwapa mitaji ya kuchimba madini kwa tija katika migodi mbalimbali nchini.

Rais wa Shirikisho la Vyama vya Wachimbaji Madini Tanzania (FEMATA), John Bina amesema hayo Jijini Arusha kwenye kikao cha wafanyabiashara wa madini kutoka mikoa mbalimbali waliokutana kujadili namna ya uanzishwaji wa benki hiyo.

Advertisement

Miongoni mwa wachimbaji waliochangia ni pamoja na mfanyabiashara, Emmanuel Wado maarufu kwa jina la ‘Sunda’ aliyetoa Sh bilioni 1 na mfanyabiashara mwingine aliyetambuliwa kwa jina la Baraka Ezekiel Nyandu aliyechangia Sh milioni 500.

Mkutano wa aina hiyo ulifanyika kwa mara ya kwanza mkoani Mwanza ambapo wachimbaji walichangishana zaidi ya Sh milioni 700 hata hivyo wataendelea kuchanga katika mikoa mingine ili kufikia mtaji wa Sh bilioni 15 kwa mujibu wa kanuni za Benki Kuu ya Tanzania (BOT).

Bina alisema uanzishwaji wa benki hiyo utajibu changamoto mbalimbali za wachimbaji na wadau wote wanaonufaika na mnyororo wa thamani ya madini.

Alitaja wanufaika kuwa ni wachimbaji madini wakiwemo wamiliki wa leseni, wenye mialo, wenye migodi, miduara, wachenjuaji, wanunuzi wa magonga ya Tanzanite, wanunuzi wakubwa wa madini na wa kati na wachuuzi.

“Mchakato wa uanzishwaji benki unahitaji maoni, uzoefu na utaalam ili kujiweka tayari hasa kununua hisa pindi benki hiyo ikianza,”amesema Bina.

Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Madini la Taifa (Stamico) Dk Venance Mwasse alisema uwepo wa benki hiyo ni maendeleo makubwa na umuhimu hasa kwa wachimbaji wadogo kwa kuwa wengi wao wanachangamoto ya mitaji. Dk Mwasse alisema wazo la uanzishaji wa benki ni zuri kwani hata mataifa mengine ya nje yataiga.

Mbunge wa Geita vijijini, Joseph Musukuma (CCM) ambaye amewawakilisha wabunge wanaotoka kwenye maeneo yenye migodi alisema uanzishwaji wa benki hiyo ni wazo zuri litakuwa kimbilio kwa wachimbaji na atamshauri Rais Samia Suluhu Hassan kuunga mkono mpango huo na kuongoza harambee ya kuchangia.

“Leo tumekutana wadau wa madini 102 tumechangishana na kupata Sh bilioni 2.8 si haba naimani ni mwanzo mzuri na hii benki itakuwa kubwa sana tunatarajia kufanya harambee  na tutamwomba Rais Samia kuongoza harambee hiyo na hii ni salamu kwa mabenki ambayo yamekuwa na ukiritimba wa kutoa mikopo na masharti magumu.”alisema

Mchimbaji maarufu wa madini ya Tanzanite, Bilionea Saniniu Laizer amesema uwepo wa benki hiyo itakuwa fursa kubwa kwa wachimbaji wadogo wengi wasio na mitaji ya kuchimba.

Mwenyekiti wa Taifa wa Chama Cha Wafanyabiashara Madini (TAMIDA),Sammy Mollel , alisema TAMIDA imefarijika kwa wazo la uanzishaji wa benki hiyo kwani  itakuwa faraja kwa wachimbaji na watakuwa wameondokana na urasimu uliopo kwenye mabenki kwa sasa.

“Tunajua faida kubwa kwa tasinia ya madini ,wachimbaji wataitumia kuhifadhi fedha watachukua mikopo isiyokuwa na riba chechefu na tutakuwa tumeondokana na urasimu” alisema Mollel

1 comments

Comments are closed.