MKUU wa Wilaya ya Kishapu mkoani Shinyanga, Joseph Mkude amewataka Wananchi wanaofanya shughuli za kibinadamu na uchimbaji wa madini kwenye eneo la Hifadhi la Bwawa la Songwa waache mara moja na kuendelea kutunza mazingira na vyanzo vya maji.
Mkude aliyasema hayo Novemba 13, 2023 wakati akizindua uwekaji wa bikoni katika eneo bwawa hilo na kupanda miti ambapo alisema wafugaji na wachimbaji wadogo wamekuwa chanzo cha uhalibifu wa mazingira kwenye bwawa hilo.
Alisema mazingira mazuri yanatakiwa kutunzwa kwani mmepata bahati ya kuwa na mabwawa mawili ni vyanzo vizuri kwa matumizi ya nyumbani na kilimo hivyo ni lazima tuyawekee mipaka ili Wananchi wasivamie.
“Rais wa jamhuri ya muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan anasisitiza uhifadhi wa mazingira na kishapu ni kame na Kampuni ya Mgodi wa Almas wa Wiliamson Diamond LTD imekuwa ikijitahidi kuzalisha miche na kuigawa bure”alisema Mkude.
Mkude alisema zoezi la kuweka mipaka limefanyika kwa lengo la kuhifadhi chanzo cha maji kisiingiliwe na mifugo wala kushughuli za kilimo ikiwemo uvuvi haramu wapo baadhi ya Wananchi walikuwa wakikataa kupanda miti sasa wameelewa na zoezi la upandaji limeenda vizuri.
Diwani wa kata ya Songwa Abdul Ngoromole alisema changamoto iliyokuwa ikijitokeza kwenye bwawa hilo kina cha maji kikipungua Wananchi wanaanza kugeuza maeneo ya kandokando kuwa eneo la kilimo na wachimbaji wadogo kuvamia wakidhani kuna almas.
“Maeneo mengi yamechibwa ndiyo maana ofisi za bonde la maji la kati wamekuja na kuweka bikoni na kutoa onyo kwa watakao halibu mazingira lakini sisi viongozi wa maeneo haya tutahakikisha tunalinda hifadhi”alisema Ngoromole.
Mwenyekiti wa kijiji cha Songwa Damas Francis alisema kijiji hicho kina wakazi 2559 ambapo alisema wako tayari kutunza na kulinda vyanzo vya maji ili visipoteze ikolojia iliyokuwepo
Mwenyekiti wa jumuiya ya watumia maji kijiji cha Songwa Zainabu Issa alisema wamekuwa wakipeana elimu juu ya utunzaji wa mazingira na maji hayo yamekuwa yakiwafaidisha kipidi cha kiangazi nakuondoa shida ya maji.
Mhandisi mazingira kutoka bonde la maji la kati Nyacheri Mramba alisema bikoni zilizowekwa ni 402 na tanki mbili zimejengwa kwaajili ya kunyweshea mifugo bila kuathiri mazingira ya bwawa pia watu wamekuwa wakilima na kuchimba madini kando ya bwawa jambo ambalo ni hatari itasababisha bwawa kukauka.