‘MKUU wa Mkoa wa Mtwara Kanali Ahmed Abbas, amewataka viongozi wa serikali Wilaya ya Nanyumbu kuwachukulia hatua za kisheria viongozi na watendaji wa vijiji wanaotuhumiwa kuiba mahindi ya ruzuku, ambayo serikali imepeleka wilayani humu kwa ajili ya wananchi wanaokabiliwa na upungufu wa chakula.

Abbas ametoa maagizo hayo mara baada ya kutembelea moja ya ghala la kuhifadhia mahindi hayo Mangaka, Wilaya Nanyumbu.
Viongozi hao wanatuhumiwa kujipatia mahindi tani 13 kwa kuandikisha majina hewa ya wananchi na kuchukua mahindi hayo na baadaye kwenda kuyauza kwa wananchi kwa bei ya juu.
“Msisitizo ni hawa waliofanya uhalifu huu, hakikisheni wanachukuliwa hatua na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria, ili kila mtu apate haki anayostahili,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Nanyumbu, Mariam Chaurembo amesema wenyeviti na viongozi sita wa vijiji walikusanya fedha na kuandikisha majina hewa ya wananchi na kujipatia mahindi hayo kwenda kuuza kwa wafanyabiashara kwa bei ya juu.
Amesema serikali ya wilaya ilianza msako na kuwakamata viongozi na wenyeviti sita wa vijiji na baadhi wananchi ambao wanatuhumiwa kujipatia mahindi ya ruzuku kwa njia ya udanganyifu na kufikishwa kwenye vyombo vya sheria.
Amesema mkoa huo ulipokea mahindi ya ruzuku kutoka serikali kuu zaidi ya tani 1,000, ambayo kwa sasa yanauzwa kwa wananchi kwa shilingi 789, huku bei ya mtaani ikiwa ni shilingi 1,500 mpaka Sh 2000 kwa kilo.