WACHUMI wametaja mambo kadhaa wanayoamini yanampa Rais Samia Suluhu Hassan uhakika wa kutekeleza ahadi ya kuboresha zaidi maslahi ya wafanyakazi.
Juzi wakati wa maadhimisho Siku ya Wafanyakazi Duniani yaliyofanyika kitaifa mjini Morogoro, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kuendelea kuboresha maslahi ya wafanyakazi kwa kurudisha nyongeza ya kila mwaka ya mishahara ya wafanyakazi pamoja na kupandishwa madaraja na kuongeza posho za safari.
Mhadhiri wa Uchumi katika Kituo cha Masuala ya China katika Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Humphrey Moshi alisema kutokana na usimamizi mzuri wa sekta za madini, maliasili na utalii unaofanywa na serikali, zinatoa hakikisho la kuongezeka kwa makusanyo ya fedha zitakazosaidia kugharamia mambo mbalimbali ya serikali yakiwamo maslahi ya wafanyakazi.
Alisema Rais Samia amekuwa hodari kuzuia ubadhirifu wa fedha za umma na kupambana na rushwa hali inayoonesha kuwa ndani ya serikali kutakuwa na matumizi sahihi ya fedha za umma na kumhakikishia utekelezaji wa ahadi kwa wananchi.
“Kitendo cha kuimarisha diplomasia ya nchi kimataifa kimemhakikishia uwezekano wa kupata mikopo kadhaa kwa riba nafuu katika kugharamia miradi mikubwa ya nchi hali itakayosaidia kutumia fedha za ndani kuwahudumia Watanzania katika masuala ya kijamii pamoja na maslahi ya wafanyakazi,” aliongeza Profesa Moshi.
Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Profesa Haji Semboja alisema hatua ya Serikali ya Awamu ya Sita kufungua milango ya uwekezaji na biashara imewezesha taifa kupata wawekezaji wengi ambao watachangia kwa kiasi kikubwa kuboresha mapato ya nchi na kuiwezesha serikali kugharamia mambo mengine ya msingi.
Profesa Semboja alisema amani na utulivu iliyopo ikichagizwa na maridhiano ya kisiasa yaliyoongozwa na Rais Samia, kwa pamoja vinatoa mazingira mazuri ya kuimarisha utendaji na kuongeza uzalishaji katika sekta mbalimbali na kuongeza mapato.
Mtaalamu wa uchumi Profesa Samwel Wangwe alisema kitendo cha kujali maslahi ya wafanyakazi, kitaongeza ari ya kazi, uzalendo na utendaji kutoka kwa wafanyakazi na kuweza kuzalisha zaidi na kuingiza mapato serikalini.
Alisema Rais Samia amejipambanua kuwa mtenda haki na fundi wa kutafuta haki kwa wale waliozipoteza.
Aliongeza kuwa Watanzania wamepata matumaini hivyo watafanya kazi kwa kujituma ili kuendana na falsafa ya Rais.
Mchambuzi na mtaalamu wa uchumi, Dk Donald Mmari alisema usimamizi mzuri wa miradi pamoja na ubunifu wa vyanzo vipya vya mapato umesababisha uwezo wa serikali wa kukusanya mapato kuongezeka hali inayoipa matumaini ya kugharamia miradi mbalimbali ya nchi.
Dk Mmari aliishauri serikali kuongeza umakini katika kudhibiti upotevu wa mapato katika halmashauri pamoja na kutumia sheria kuweka nidhamu ya matumizi ya fedha za umma katika kugharimia miradi mbalimbali.
Aliwashauri wafanyakazi kutambua nia na madhumuni ya Rais Samia ya kujenga mazingira bora ya maisha yao kwa kuboresha maslahi yao hivyo kuwataka kufanya kazi kwa bidii, maarifa na ubunifu ili kumfanya Rais Samia kutimiza ahadi yake kwa wepesi.