WAKAZI wanaopakana na Kiwanja cha Ndege cha Shinyalu mjini Kakamega, wanadai fidia ya makaburi kabla ya kuhamishwa kupisha upanuzi ili kuruhusu kufikiwa kwa ndege kubwa za kibiashara.
Desemba 2022, Rais William Ruto aliidhinisha kiwanja hicho baada ya kufanyiwa ukarabati wa njia ya kurukia ndege, barabara ya teksi na uboreshaji mwingine kwa gharama ya Sh milioni 174.7.
Wakazi hao walinukuliwa wakisema mizimu ya mababu zao itawaandama popote watakapohamia kama hawataiheshimu kwa kuacha makaburi yao mikononi mwa wageni.
Walisema serikali haina budi kuwalipa ili wawe na rasilimali za kuwasaidia kukidhi gharama ya kufanya ibada kuwatuliza mababu zao waliofariki kabla ya kuondoka eneo hilo.
“Mila hazituruhusu kuhamia mahali pengine kama ardhi tuliyorithi kutoka kwa mababu zetu ina makaburi yao,” alisema Oscar Musonye.
Aliongeza, “kuna ibada ambazo lazima zifanyike juu ya makaburi kabla ya kuondoka ikiwa ni njia ya kuwasiliana na kutuliza roho za mababu zetu.”
Serikali katika Kaunti ya Kakamega imewashirikisha machifu na wasaidizi wao kuwaelimisha wakazi hao umuhimu wa kiuchumi na kijamii wa kupanua uwanja huo.
Chifu Msaidizi wa Shiswa, Bernard Shikhovolo, alisema fedha nyingi zitahusika katika mchakato wa kufidia. “Inabidi tuwaelimishe (wananchi) jinsi ya kuzitumia kwa uangalifu ili kuziweka upya na kuepuka vishawishi vya kuzitumia kwa anasa.”
Madai yao yanakuja siku chache baada ya Serikali ya Kaunti ya Kakamega kutoa pendekezo la kuwahamishia wakazi hao katika msitu wa Shikutsa na Kakamega kupisha upanuzi wa uwanja huo ili kuruhusu kufikiwa kwa ndege kubwa za kibiashara.