Wadau kuungana na Serikali upatikanaji wa maji

WADAU wa maji na mazingira wamesema ipo haja ya serikali na wadau wengine kuunganisha nguvu pamoja kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za maji,usafi wa mazingira na uzoaji wa taka ili kuboresha makazi yao.

Akizungumza kwenye maadhimisho ya Siku ya Choo duniani, jijini Dar es Salaam Mkurugenzi Mkazi wa Shirika la Water Aid Anna Mzinga amesema maji na usafi wa mazingira ni mambo mawili ambayo yanaingiliana, na haiwezekani ushughulikia moja bila nyingine.

Mzinga amesema katika maadhimisho hayo ya Siku ya Choo duniani, wadau wa maji, usafi wa mazingira na serikali wanawajibu wa kuunganisha nguvu pamoja kuhakikisha miundombinu ya wananchi kupata huduma hizo inaboreshwa na kila kaya iwe na choo bora.

“ Kuwa na mifumo bora ya usafi wa mazingira haisaidii tu kuzuia kuenea kwa magonjwa yanayotokana na maji, bali pia kunalinda maji ya rdhini kutokana na athari mbaya za usafi wa mazingira,”alisema Mzinga.

Akitaja takwimu amesema asilimia 33.5 ya kaya Tanzania Bara za mjini vyoo vyake vimeboreshwa na kwa upande wa vijijini vyoo vilivyoboreshwa ni asilimia 8.9 tu ya kaya.

Kadhalika, upande wa mjini asilimia 70 hadi 80 ya wananchi hawana huduma bora za miundombinu ya usafi wa mazingira na ukusanyaji wa taka.

Kuhusu mifumo bora ya maji taka na usafi wa mazingira, ripoti zinaonesha kuwa miji na majiji 10 tu yana mifumo bora ya maji taka ambayo yanachukua asilimia 20 ya idadi ya watu.

“Hii inaonesha hatua zaidi zinatakiwa kuchukuliwa kuboresha muindombinu ya maji taka kwenye maeneo ya miji na majiji,”amabainisha Mzinga.

Amesema mwaka 2021 WaterAid kwa kushirikiana na Wizara ya Afra, walifanya utafiti kwenye maeneo ya kazi kuangalia ubora wa mifumo ya maji taka na usafi wa mazingira katika sekta isiyo rasmi mkoani Dar es Salaam,Dodoma na Arusha.

Matokeo ya utafiti huo yalibaini kuwa wafanyakazi wa sekta isiyo rasmi wako kwenye hatari ya majanga na maradhi kutokana na mazingira duni na huduma hizo muhimu.

Hivyo katika kuadhimisha Siku ya Choo duniani, shirika hilo limesema litaendelea na juhudi zake kusaidia upatikanaji wa huduma bora ya maji, vyoo bora na miundombinu imara ya majitaka ili kuhakikisha wananchi wanakuwa salama kuepuka maradhi.

Ametoa mwito kwa wadau wengine kushirikiana na serikali kusaidia maeneo na jamii zenye huduma duni ya mifumo ya majitaka kuyaboresha katika kukabiliana pia na mabadiliko ya tabianchi.

 

Habari Zifananazo

Back to top button