Wadau madini watakiwa kuelewa mikataba

ARUSHA: Wadau wa sekta ya madini nchini wametakiwa kusoma na kuelewa mikataba mbalimbali wanayopewa katika makubaliano kabla ya kuisaini, hususani katika taasisi za bima.

Hayo yamesemwa leo Mei 23, 2024 na Meneja wa TIRA Kanda ya Kaskazini, Bahati Ogolla katika Jukwaa la Tatu la Ushirikishwaji wa Watanzania katika sekta ya madini linaloendelea kwenye Ukumbi wa Kimataifa wa Mikutano (AICC) jijini Arusha.

Jukwaa hilo linalofanyika kila mwaka limeandaliwa na Serikali kupitia Tume ya Madini chini ya Wizara ya Madini, likiwa na lengo la kukutanisha wadau mbalimbali kutoka sekta ya madini kujadili na kufanya tathmini ya ushirikishwaji wa Watanzania katika mnyororo wa sekta hiyo.

Akizungumza Ogolla amesema kuwa wananchi wengi wanakutana na changamoto mbalimbali ya mikataba kwa kuwa wanaisaini bila kusoma na kuielewa.

“Someni mikataba vizuri kama huelewi tumia wanasheria au njoo TIRA kwa msaada zaidi, msiingie mikataba bila kujua faida na hasara,”amesema.

Amesema kabla ya kuisaini ni vyema kushirikisha baadhi ya watu, ili kushauriana na kuepuka matatizo na maumivu yatakayojitokeza baadaye.

TIRA imetoa mapendekezo nane ya kufuatwa ili Watanzania waweze kunufaika na huduma za bima.

Mapendekezo hayo yaliyotolewa ni pamoja na wananchi kuhakikisha shughuli na mali zinawekewa kinga dhidi ya vihatarishi mbalimbali, kuhakikisha wanalipa ada za bima inavyotakiwa na kuhakikisha wanatambua haki na wajibu wao kwenye mkataba wa bima mfano ukomo wa muda wa kuwasilisha madai na uwasilishaji wa vielelezo vinavyotakiwa.

Mapendekezo mengine ni pamoja na kuhakikisha kwamba wanatambua kanuni na taratibu za bima ikiwemo ulipaji wa ada ya bima, uaminifu uliotukuka, uhusiano wa umiliki wa mali na mkata bima kurejeshwa kwenye hali iliyokuwepo kabla ya janga kutokea.

 

Habari Zifananazo

Back to top button