Wadau utalii kuanza kupokea mikopo

WADAU wa sekta ya utamaduni na sanaa wanatarajia kuanza kupokea mikopo mwezi Agosti mwaka 2023.

Akitoa taarifa hiyo siku ya leo, Julai 13, 2023 jijini Dar es Salaam waziri wa Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Pindi Chana amesema mikopo hiyo itatolewa kupitia taasisi za fedha za benki ya NBC na CRDB katika mikoa yote nchi nzima.

Balozi Chana ametoa taarifa hiyo wakati akifungua warsha ya kuwajengea uwezo viongozi wa mashirikisho ya utamaduni na sanaa, ambapo amewataka kufikisha ujumbe sahihi kwa wanachama wao ili waelewe vyema lengo la mkopo huo na faida zake katika kazi zao za utamaduni na sanaa.

Aidha Waziri huyo aliyaagiza mashirikisho ya utamaduni na sanaa benki ya NBC na mfuko wa utamaduni na sanaa kufanya kazi kwa kushirikiana katika utekekezaji wa mpango huo wa serikali kuanzia hatua ya awali ya utoaji wa mikopo hadi ufuatiliaji wa marejesho.

Kwa upande wake Mwakilishi wa Mtendaji Mkuu wa Benki ya NBC Elvis Ndunguru amesema benki hiyo itakopesha mtu mmoja hadi shilingi milioni 100 kwa riba ya asilimia tisa ambayo ndio riba ya chini sokoni.

Aidha, Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko huo, Nyakaho Mahemba amesema lengo la kutoa mafunzo hayo ni kuwasaidia Wadau hao kuelewa vigezo vya kupata mkopo na namna ya kutumia mikopo hiyo.

Habari Zifananazo

Back to top button