DAR ES SALAAM: WADAU wa Demokrasia kutoka ndani na nje ya nchi wameitaka Tume ya uchaguzi nchini (NEC)kudhibiti vitendo vya rushwa katika vyama vya siasa ili kutoa fursa kwa watu wengi hususani wanawake kugombea.
Hayo yamesemwa leo Januari 6, 2023 na Mwanasiasa mkongwe Getrude Mongela katika mjadala wa utoaji maoni ya miswada ya sheria ya uchaguzi, vyama vya siasa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi.
Mongela amesema sheria zinazoenda kupitishwa hata zikiwa nzuri kiasi gani bila kuondoa rushwa ni kazi bure na wanawake hawatopata nafasi.
“Wengine kipindi chetu tuliomba nafasi kama omba omba, hakukua na rushwa ya ngono wala ya fedha, ni kujinyenyekeza tu na kuonyesha uwezo wa kujieleza, lakini sasa hivi rushwa imetamalaki, hili liangaliwe, lidhibitiwe, ” amesema Mongela na kuongeza
” Hata mwanamke anayepewa nafasi awe na uwezo sio kwa sababu ya undugu, urafiki, ” amesema.
Aidha, amesema nafasi ya mwanamke katika uongozi ni lazima na si ombi wala hisani litekelezwe kwa mujibu wa sheria.
“Usawa unaleta uhuru, uwezi kuwa huru kama unanyanyaswa, hupati fursa sawa, tume iangalie chama kisichotekeleza idadi ya wanawake, kisipewe nafasi wajue kabisa kuna adhabu kali.
Nae, Mbunge wa Viti Maalum, Neema Lugangira akichangia amesema Tume ya Uchaguzi iweke mfumo mzuri wa kusimamia fedha zinazotumika kujengea uwezo wanawake.
Pia ametaka ibara ya 112 na 113 ya sheria ya uchaguzi iweke namna nzuri ya kuwapata wabunge na madiwani wa Viti Maalum.
“Hii itasaidia kuimarisha na kupambania na ukatili wa kijinsia ndani ya vyama ya siasa,” amesema Neema.
Aidha, amependekeza kuweka na madawati ya jinsia kwenye vyama vya siasa kwa kushirikiana na Msajili ili awe na meno kuchua hatua ukiukwaji unapotokea.
Pia, amesema sheria itambue matukio ya ukatili ibara ya 60 (1) iongezwe kosa la ukatili wa kijinsia kwenye mitandao ya kijamii na ukatili wowote ule mtu anayehusika iwe moja ya kumuondoa katika nyanja za siasa katika kipindi chote iwe ni kwenye uchaguzi hata baada ya uchaguzi.