Wadau wa haki jinai wanolewa mashauri ya wanyamapori

CHUO cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) kwa kushirikiana na Mahakama ya Tanzania watatumia siku tano kuwajengea uwezo wadau wa haki jinai kuhusu namna iliyo bora ya uendeshaji mashauri dhidi ya wanyamapori kwa kuzingatia sheria, weledi na uadilifu ili kusaidia viumbe hao wasitoweke.

Majaji wa Mahakama Kuu pamoja na mahakimu, waendesha mashtaka na wapelelezi waandamizi ni sehemu ya wadau wa haki jinai wanaoshiriki mafunzo hayo yaliyofunguliwa leo mjini Iringa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Iringa, Ilvini Mugeta.

Mafunzo hayo yanayofadhiliwa na taasisi inayojishughulisha na uhifadhi wa mazingira na usalama wa wanyamapori ya PAMS Foundation ni mtiririko wa mafunzo mengine kama hayo yaliyofanyika jijini Arusha, Morogoro na Katavi kwa nyakati tofauti kati ya mwaka jana na mwaka huu.

“Mafunzo haya yanawaleta pamoja wadau wa utoaji haki jinai na watabadilishana uzoefu katika kupeleleza na kushughulikia makosa dhidi ya wanyamapori kwa kuzingatia sheria za kitaifa na kimataifa,” Jaji Mugeta alisema.

Aidha alisema mafunzo haya yatawawezesha wapelelezi namna ya kufanya upelelezi kama sheria inavyotaka ili kuwezesha kesi zinapofikishwa mahakamani na waendesha mashitaka ziwe na ushahidi wa kutosha utakaowatia hatiani wakosaji.

Alisema wadau wote wanaoshiriki katika sekta ya uhifadhi wana wajibu wa kuwalinda dhidi ya ujangiri wanyamapori na viumbe vingine ikiwemo misitu kwa kuzingatia misingi ya sheria.

“Kwa takwimu tunaambiwa kuna aina milioni 10 za wanyamapori na mimea na kati yake aina 3,000 zipo katika hatari ya kupotea. Kwahiyo ni lazima hatua zichukuliwe ili viumbe hivyo visipotee,” alisema.

Mkurugenzi wa Mafunzo na Uendeshaji wa PAMS Foundation, Samson Kassala alisema mahakama inapaswa kushirikiana na wadau wake kuhakikisha sheria imara za uhifadhi na mifumo ya haki inasimamiwa ipasavyo na kushughulikia ukiukwaji wa sheria hizo.

Kassala alisema PAMS Foundation imekuwa ikisaidia katika kuwajengea uwezo walinzi wote wa maliasili za Taifa ili watekeleze majukumu yao kwa ufanisi na kwa manufaa ya wananchi na vizazi vijavyo.

Mmoja wa wakufunzi wa mafunzo hayo, Mhadhiri Msaidizi wa IJA, Roggers Cletus alisema makundi hayo yameshirikishwa kwenye mafunzo hayo kwa kuwa kila kundi lina wajibu wake katika kuhakikisha Mashauri yanakwenda vizuri mahakamani.

Kwa kupitia mafunzo hayo alisema washiriki hao watafundishwa sheria ya wanyamapori, uchunguzi wa masuala ya wanyamapori na misitu, utekelezaji wa amri za mahakama, na utunzaji utoaji na uharibifu wa vielelezo vikiwemo vya kimtandao.

Mratibu wa mafunzo hayo Patrisia Kisinda alisema mafunzo hayo ni muhimu kwa kuwa bado kuna vitendo vingi vya ujangili vinaendelea kutokea katika maeneo mbalimbali nchini na kufikishwa mahakamani.

Alisema matarajio yao ni kuona wanufaika wa mafunzo hayo wana kuwa na uwezo zaidi wa kuendesha kesi kwa manufaa ya Taifa na kwa ulinzi wa maliasili zilizohifadhiwa kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo.

 

Mwisho.

Habari Zifananazo

Back to top button