Wadau wa reli waomba muda wa leseni kuongezwa
Lengo ni kuongeza wawekezaji zaidi
DAR ES SALAAM: WADAU wa masuala ya reli wameomba kanuni mpya za reli ziongeze muda wa leseni kwa watoa huduma binafsi kwani muda wa miaka mitano ni mdogo ikilinganishwa na uwekezaji unaotakiwa.
Aidha, Wizara ya Uchukuzi imewataka wadau wengine kuendelea kutoa maoni yao ndani ya siku 14 kuhusu rasimu kabla ya kusainiwa kwa kanuni mpya za reli.
Mku wa Kitengo cha mnyororo wa thamani wa Shirika la Mpango wa Chakula Duniani (WFP) Mahmud Mabuyu amesema endapo kipengele hicho hakitabadilishwa, wawekezaji wataona kuwa ni hatari kuwekeza katika eneo hilo.
Akizungumza katika mkutano wa kukusanya maoni ya wadau kuhusu rasimu ya kanuni za watoa huduma binafsi leo Dar es Salaam, Mabuyi amesema uwekezaji wa reli ni tofauti na sehemu nyingine kwa sababu mabehewa na injini zinatumia miaka 15 na zaidi mpaka ifikie hatua ya kubadilishwa na gharama yake ni kubwa hivyo muda wa miaka mitano hautoshi.
Amesema “Napendekeza kufanyiwa marekebisho kwa kipengele hicho kwani itakatisha tamaa wawekezaji, wataona kuna hatari ya kuwekeza eneo hili hivyo watakimbia.”
Pia amesema wamependekeza kuwepo kwa msimamizi binafsi wa reli ambaye atasimamia waendeshaji wote wa reli hiyo kuliko kuacha Shirika la Reli Tanzania (TRC) kama msimamizi na muendeshaji.
Ameeleza kuwa lipo soko kubwa katika kutumia reli lakini uwezo wa reli ya Mitageji MGR unapaswa kufanyiwa tathmini mpya kabla ya kutangaza kwa wadau ili kujua kama reli hiyo bado inauwezo wa kubeba tani milioni tano kwa mwaka au umepungua.
Amesema kuwa shirika hilo limekuwa mdau mkubwa wa TRC na kwamba wameridhika kwa kushirikishwa kabla ya kutumika kwa kanuni hizo.
Mapendekezo mengine wametaka kanuni hizo zieleze wazi kama mtoa huduma anaweza kuwa na waendeshaji wake au watatumia wa shirika hilo.
Mkurugenzi wa Mamlaka ya Usafiri Ardhini (Latra), Habibu Suluo amesema Sheria ya TRC haikuruhusu watoa huduma binafsi kushiriki katika uendeshaji wa reli hiyo.
Amesema katika tathimini iliyofanywa na mamlaka hiyo kuangalia mchango wa reli katika kuondoa mizigo bandarini imebaini kuwa ni asilimia 1.3 pekee ya mizigo husafirishwa na reli na iliyobaki inatumia malori.
“Ni wakati muafaka wa kuhakikisha maboresho na uwekezaji katika miundombinu hii kuwezesha mizigo iondoshwe kwa haraka,” ameeleza Suluo.