Wadau wa usafiri wapinga viwango vya nauli za SGR

WADAU wa masuala ya usafiri nchini wamepinga viwango vya nauli za abiria zilizopendekezwa na Shirika la Reli Tanzania (TRC) kwa treni ya Kisasa ya Standard Gauge (SGR) kwamba hazijazingatia uchumi wa Watanzania wenye hali ya chini ambao ndio watumiaji wakubwa wa usafiri huo.

Hata hivyo, wamependekeza nauli za SGR kutoka Dar es Salaam hadi Morogoro iwe Sh 8,000 kwa abiria mwenye umri zaidi ya miaka 13 badala ya Sh 24,794 na chini ya miaka hiyo iwe Sh 4,000 wakati TRC imependekeza Sh 12,397 kwa daraja la kawaida na 14,876 kwa daraja la kati.

Aidha, wamependekeza nauli kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma iwe Sh 19,000 hadi Sh 24,000 kwa mtu mzima badala ya Sh 59,494 na mtoto iwe Sh 9,000 badala ya Sh 29,747 na 35,696.

Wakizungumza Dar es Salaam jana katika mkutano wa kupokea maoni ya wadau kuhusu viwango vya nauli za abiria kwa treni ya SGR ulioandaliwa na Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Ardhini (LATRA), wadau hao wamesema endapo nauli zitakuwa chini zitavutia idadi kubwa ya watu kutumia usafiri huo na kuongezeka kwa biashara.

Kaimu Katibu Mtendaji wa Baraza la Ushauri wa Watumiaji wa Huduma za Usafiri Ardhini (LATRA CCC), Leo Ngowi alisema baada ya mapendekezo hayo walihoji watu 53 ikiwa wanaridhika nauli zilizoombwa au la na kwamba asilimia 100 walionesha kutoweza kulipa nauli hizo kwa mikoa hiyo.

Alisema mapendekezo ya TRC ni kutaka kutengeneza faida kubwa ambayo ni zaidi ya gharama za chini au wastani za uendeshaji na kwamba inafurahia kutokuwa na mshindani.

Pia alisema kuwa kwa nauli iliyopendekezwa hakutakuwa na abiria wa kutumia SGR hivyo wanapaswa kuomba ruzuku serikalini kwa ajili ya kugharamia wafanyakazi, gharama za mifumo ya reli na uendeshaji ili kumwezesha abiria kulipa gharama nafuu na wao kutoa huduma bora za usafiri.

Mkuu wa Wilaya ya Ilala, Ng’wilabuzu Ludigija aliitaka Latra kutokubali mapendekezo ya TRC mpaka itakapojiridhisha na huduma zitakazotolewa na shirika hilo, kasi ya treni na kufanya mapitio ya nauli katika nchi nyingine kama zinaendana na viwango hivyo.

Alitaka treni hiyo itakapoanza, kuwepo na nauli za mpito ambazo Watanzania wote wataweza kuzimudu hivyo utakuwa muda mzuri wa kuangalia huduma za treni hiyo.

“Mjipe muda wa kutosha kabla ya kutangaza nauli halisi, muangalie Kenya na maeneo mengine wanafanyaje na nauli zao zikoje kwa sababu matamanio ya serikali ni kuona kila mwananchi anamudu kupanda treni ya SGR,” alisema.

Alifafanua kuwa TRC inapaswa kutambua kuwa usafiri wa treni ni wa Watanzania wenye kipato cha chini, hivyo mapendekezo yao yawaangalie wakulima wadogo wa pamba na mawese sambamba na kuzingatia maoni ya wananchi yanayotolewa.

Mwananchi Sudy Mohamed alisema kuwa bei za nauli zingeshuka zaidi kwa sababu ya kuangalia uchumi wa mtu mmoja mmoja.

“Napendekeza nauli ya Dar es Salaam hadi Morogoro inapaswa iwe 8,000 na kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma iwe kuanzia shilingi 20,000 hadi 24,000 kutokana na hali za watumiaji wa usafiri huu,” alisema.

Kwa upande wake, Kaimu Mkurugenzi wa Biashara na Maendeleo wa TRC, Fredrick Massawe alisema wameangalia maeneo matano ya uwekaji wa viwango vya nauli hizo ikiwemo kutoweka gharama za miundombinu ya reli, muda na kasi ya treni na ukarabati.

Alisema endapo wangeingiza gharama hizo kwa asilimia 100, nauli kutoka Dar es Salaam hadi Dodoma ingekuwa zaidi ya Sh 200,000.

“Usafiri huu unategemea kuwa na abiria 1,990,656 kwa mwaka, pia treni hii itakuwa na safari sita kwa siku kwani itatumia chini ya saa mbili kufika Morogoro na ukilinganisha na nchi nyingine treni yetu itakuwa inaenda kasi zaidi na kwa gharama nafuu, hivyo itaongeza faida kwa abiria kufika kwa wakati, kupunguza uchafuzi wa mazingira kwa kutumia mafuta na gharama za ukarabati wa miundombinu ya barabara,” alisema.

Aliongeza kuwa hawategemei abiria kuwa ndio watarudisha faida ya uwekezaji wa mradi huo badala yake wanategemea usafirishaji wa mizigo zaidi ili shirika liweze kujiendesha na kupata faida.

Naye Mkurugenzi wa Latra, Habibu Suluo alisema wanaendelea kupokea maoni ya wadau hadi Januari 3, 2023 ili kufanya maamuzi kwa viwango hivyo ambavyo vimeleta mtafaruku.

Alisema walipoweka mapendekezo hayo, Watanzania wengi walidhani kwamba ndio nauli zilizopitishwa na mamlaka hiyo lakini kwa mujibu wa sheria wanapaswa kuitisha kikao na wadau ili kujadiliana.

Habari Zifananazo

Back to top button