Wadau wajadili vizingiti vya utalii ukanda wa Kagera

WADAU wa utalii kupitia maonesho ya kibiaahara uwekezaji na utalii East Afrika Expo yanayoendelea mkoani Kagera wamefanya kongamano la kujadili namna ya kuondoa vizingiti/vikwazo kwa pamoja vinavyokwamisha utalii katika ukanda wa Kagera .

Kangamano hilo lililoandaliwa na kampuni ya utalii ya Kiroyera Tours na kuongozwa na Rais wa Bodi ya Utalii Afrika, Cuthbert Ncube lililenga kujadili kwa pamoja vizingiti vilivyopo katika kukuza utalii Ukanda wa Kagera na maeneo yaliyouzunguka mkoa huo pamoja na ushiriki wa wadau katika kutangaza vivutio vya utalii vinavyopatikana.

Katika ufunguzi wa kongamano hilo,  Ncube alisema ili kukuza utalii wa Afrika kwa ujumla waafrika wanapaswa kuanza kwa kuiuza Afrika kama kivutio cha utalii kwa mataifa mengine.

Advertisement

“Changamoto za maswala ya utalii kwa mikoa ambayo haijachangamka kiutalii zinafanana Katika bara la Afrika na kila mmoja ukimuulizia atakwambia miundombinu sio mizuri lakini kwa pamoja wadau wa utalii tunapaswa kujiuliza ni lini tumegeuka kuwa na ushawishi kwa wageni ambao hawajawai kufika maeneo yetu na kuwaeleza uzuri wa maeneo Yetu na vitu vya kipekee vinavyopatikana na jinsi vinavyovutia ?! Alihoji Ncube.

Alisema kuwa Wananchi wengi na wadau wengi kutoka katika nchi za Afrika wanawaza kwenda nje kutembea na kufurahia madhari katika nchi za nje lakini ukwelkwamba bado hawajafanya utafiti na uchunguzi wa kutosha kuhusu madhari na upekee wa vivutio vinavyofurahisha kutoka katika nchi zao hivyo watu pekee wa kubadilisha fikra zao ni wadau wa utalii.

Mhadhiri wa Chuo Kikuu Cha Dare es salaam ambaye ni mdau wa utalii,  Dr Frolence Rutechura alisema kuwa Mkoa wa Kagera umebahatika kuwa na vivutio vingi ikiwemo ziwa Victoria ,misitu ,kupakana na nchi za Afrika Mashariki michoro ya mapangoni lakini utalii haujachangamka kwa sababu ni watu wachache ambao wanaelezea utalii uliopo.

Alisema ni wakati wa wadau na makampuni ya utalii kubadilika kwani si kutokuwepo kwa miundombinu mizuri sio kizingiti pekee kinachosababisha ukosefu wa watalii mkoani Kagera isipokuwa bado watu wengi kutoka mikoa mingine na nchi nyingine hawajaelezwa vya kutosha kuhusu upekee wa vivutio vilivyoko mkoa wa Kagera.

Mkurugenzi wa Kampuni ya utalii ya Kiroyera Tours Mary kalikawe alisema mkoa wa Kagera unapata watalii kutoka nje wachache ambao wanaweza wasivuke 1,000 kwa mwaka lakini Kongamano hilo limeweka mipango madhubuti ya kubainisha vivuto vipya vya utalii na namuna ya kuvitangaza.

Alisema mkoa huo unasifika kuwa na vivutio vya kipekee ikiwemo fukwe za ziwa victoria, visiwa , misitu inayovutia,mbuga za Wanyama ,mipaka mingi,miti ya asili hivyo baada ya kongamano ni kuja na mtizamo mpya wa kutangaza vivutio hivyo kwa wadau ili wakazi wa mkoa huo kuonja matunda ya utalii.

Kongamano hilo limewahusisha wadau mbalimbali wa utalii yakiwemo makampuni ya utalii, wasomi wa vyuo vikuu ,wadau wa utalii ambao ni wasomi wasitaafu, wanafunzi wa vyuo vya Kati kutoka mkoani Kagera wanaosomea maswala ya utalii, wadau wa mazingira pamoja na wadau wa utalii kutoka nchi za Afrika Mashariki ambao wameshiriki maonyesho ya kibiashara, uwekezaji na utalii yanayoendelea mkoani Kagera.

3 comments

Comments are closed.