WACHAMBUZI wa masuala ya kidiplomasia na kisiasa wamesema Rais Samia Suluhu Hassan amefanya jambo muhimu kutangaza siku tano za maombolezo ya kifo cha Malkia Elizabeth II wa Uingereza.
Malkia Elizabeth II wa Uingereza aliaga dunia Septemba 8 mwaka huu nchini Scotland na anatarajiwa kuzikwa Septemba 19, mwaka huu.
Taarifa iliyotolewa Septemba 10 mwaka huu na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais Ikulu, ilieleza kuwa maombolezo hayo yalianza siku hiyo hadi Septemba 14.
Wachambuzi walisema uamuzi wa Rais Samia utaimarisha uhusiano wa kidiplomasia na kiuchumi kati ya Tanzania na Uingereza na nchi nyingine.
Mchambuzi wa masuala ya diplomasia na siasa wa Chuo cha Diplomasia Kurasini Dar es Salaam, Abbas Mwalimu, alisema kitendo cha Tanzania kuomboleza kifo cha Malkia Elizabeth II ni sehemu ya utamaduni wa kidiplomasia na kimataifa.
Mwalimu alisema Tanganyika haikuwa koloni la Uingereza ila mwaka 1919 Umoja wa Mataifa (UN) kupitia Baraza la Udhamini uliiamuru Uingereza iyaweke makoloni yote ya Ujerumani chini ya uangalizi wake baada ya Ujerumani kushindwa katika Vita ya Kwanza ya Dunia mwaka 1918 hivyo Tanganyika ikapata uhuru wake kutoka mikononi mwa Waingereza.
Jana katika kongamano la wanawake na vijana wa eneo huru ya biashara Afrika (AfCFTA), Rais Samia alizungumzia kifo cha Malkia na akataka wajumbe wasimame kwa dakika moja kuomboleza.
“Uingereza ni nchi ambayo tuna mfungamano nayo wa kihistoria, pia imetufanya tukawa wanachama wa Jumuiya ya Madola, kwa hiyo tunatambua tuko katika mwavuli mmoja, hivyo lazima tumpe Malkia heshima hiyo na kwa heshima hiyo, serikali imetangaza siku tano za maombolezo,” alisema Mwalimu.
Pia alisema Uingereza inaongoza kwa uwekezaji Tanzania lakini pia ni mbia wa maendeleo, hivyo kitendo cha Tanzania kuweka siku tano za maombolezo kutafanya Waingereza waone namna Tanzania inavyowathamini.
Kwa mujibu wa Mwalimu, miongoni mwa mambo ambayo Malkia Elizabeth II ameyaacha kama alama ni pamoja na Jumuiya ya Madola aliyoianzisha wakati wa utawala wake, Uingereza kukua kiuchumi na kuwa nchi ya tano yenye uchumi mkubwa duniani, alikuwa alama ya umoja wa kitaifa na kimataifa na mpenda amani.
Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda alisema moja ya malengo ya nchi yoyote duniani ni kuendeleza uhusiano mzuri na nchi nyingine kidiplomasia, hivyo uamuzi wa Tanzania kuomboleza kifo cha Malkia ni muhimu katika kukuza uhusiano huo.
Dk Mbunda alisema Tanzania inashirikiana vizuri na Uingereza na kuna misaada ambayo Uingereza inaendelea kutoa kwa Tanzania.
Mwenyekiti wa Chama cha Democratic Party (DP) Taifa, Philipo Fumbo, alisema kwa kuwa Uingereza iliitawala Tanganyika na ilitoa uhuru kwa Tanganyika, hivyo uamuzi wa Rais Samia wa kutangaza maombolezo hayo ni heshima kwa Malkia na siyo kitu kibaya.
“Mimi ninavyoona ni sawa kwa heshima ya Malkia, ni mama ambaye ameiongoza nchi ya Uingereza kwa miaka 70, kwa hiyo siyo kitu kibaya. Nchi za Jumuiya ya Madola zimuenzi Malkia kwa kukomesha biashara haramu ya binadamu kwa kuwa Malkia alipinga biashara ya utumwa,” alisema Fumbo.