KUELEKEA msimu wa tatu wa tuzo za harusi 2023 ‘Harusi Awards 2023’ waandaji wa tuzo hizo ambazo ni sehemu ya maonyesho ya biashara ya harusi ‘Harusi Trade Fair’ wameomba sekta ya harusi nchini irasimishwe kutokana na mchango wake mkubwa kiuchumi ndani ya jamii
Kauli hiyo imetolewa hii leo Mei 22, 2023 jijini Dar-es-salaam na Benedict Msofe katika mkutano na waandishi wa habari kwa niaba ya waandaji wengine wa tuzo hizo zilizopangwa kufanyika Mei 28, 2023 hotelini hapo
“Sekta ya harusi imekuwa na imegeuka kuwa biashara rasmi, wastani ya harusi 350 husherehekewa ndani ya Juma moja kwa Dar-es-salaam pekee hivyo kutoa maelfu ya fursa za ajira kwa wanawake na wanaume. Tunakusudia kukuza wafanyabiashara wa harusi na watoa huduma ili kueneza biashara na kuipa ubora sekta ya harusi nchini Tanzania”
Kwa upande wake Bahiya Tajiri, mmoja wa waratibu wa tuzo hizo amesema wamejidhatiti kusimamia haki, uwazi, usawa na ubora katika mchakato mzima wa kufanikisha tuzo hizo
“Zile taarifa ambazo jopo la majaji watazipata zinapaswa zisiwe na upendeleo. Pia tumejipanga kuhakikisha weledi katika upigaji kura kwa njia ya kielektroniki .”
Naye Lilian Mduda meneja masoko na mawasiliano wa hoteli ya Hyatt Regency, The Kilimanjaro ya jijini Dar-es-salaam ukumbi ambao ‘Harusi Awards 2023’ itafanyika amesema wamejidhatiti kutoa huduma bora kwa wageni wote watakaohudhuria hafla hiyo
Itakumbukwa tuzo za mwaka huu ni awamu ya tatu ya tuzo hizi za maonyesho ya biashara ya harusi katika kutambua mchango wa wachuuzi wa harusi na watoa huduma nchini
Tuzo za mwaka huu zimegawanywa katika vipengele 19 ikiwemo ukumbi bora wa mwaka, mpambaji bora wa mwaka, DJ wa harusi wa mwaka na vipengele vingine ambapo kipengele kinachotarajiwa kuwa na mchuano mkubwa ni kile cha mshereheshaji (MC) bora wa mwaka.j