Wadau wapongeza tamasha la SensaBika

MASHABIKI na wadau wa sanaa na michezo mbalimbali wameipongeza serikali kwa kuandaa tamasha la ‘SensaBika’ kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni Dar es Salaam.

Tamsha hilo lililoandaliwa na Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo ikishirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) lenye lengo la kuhamasisha Sensa ya Watu na Makazi itakayofanyika kesho nchi nzima.

Akizungumza na gazeti hili katika viwanja hivyo, Meneja wa Msondo Ngoma, Said Kibiriti ambaye pia ni Katibu wa Chama cha Muziki wa Dansi Tanzania (Chamudata), alisema tamasha hilo limefana kutokana na mapokezi mazuri ya watanzania na sanaa na michezo kiujumla.

Aidha, Kibiriti alisema Sensa ya Watu na Makazi ni muhimu ili kutambua idadi ya watu waliopo katika eneo fulani na Serikali ijue inapeleka huduma kwa watu wangapi kwenye eneo hilo. “Ili bajeti iende vizuri ni muhimu kuhesabiwa na kupata idadi kamili ya watu,” alisema Kibiriti.

Mwigizaji wa maigizo, Bakari Mbelemba ‘Mzee Jangala’ alisema jambo walilofanya serikali ni muhimu kwa kukutanisha sanaa mbalimbali na michezo ili kuhamasisha sensa. Alisema sanaa ni chanzo cha kutoa elimu na kuelimisha juu ya jambo fulani katika jamii, hivyo ni wajibu wa wasanii kufikisha ujumbe kupitia vipaji vyao.

“Pongezi kwa serikali kwa kuandaa jambo hili, kwani ni muhimu kwa wasanii kutoa elimu kwa watanzania, pia Sensa ya Watu na Makazi ni msingi imara ya kuboresha taifa kupitia idadi iliyopo nchini watanzania wanapaswa kutoa ushirikiano kwa makarani,“ alisema.

Upande wa mratibu wa sensa Mkoa wa Dar es Salaam, Alberto Mapala alisema maandalizi ya sensa mkoa wake yamekamilika na sasa wanasubiri siku ifike ili kufanya kazi ya kuhesabu watu na kupata idadi kamili.

Mwanamitindo, Caroline Mwakasaka ambaye alikuwa mshindi wa kwanza katika mashindano ya urembo ya Afrika kwa watu wenye ulemavu wa kusikia yaliyofanyika mwaka jana, alitoa wito kwa waiosikia ‘viziwi’ kujitokeza kwa wingi katika sensa.

“Wito kwa watanzania hasa viziwi kujitokeza na kutoa ushirikiano kwa makarani ili kupata idadi kamili, “ alisema. Rais wa Shirikisho la Sanaa na Maonyesho nchini, Cynthia Henjewele alisema wanashukuru kuona wasanii walijipanga kutoa burudani nzuri na kuhamasisha Sensa kwani kazi ya sanaa ni kutoa elimu na kuelemisha kupitia vipaji walivyokuwa navyo.

“Tunashukuru tumefanikisha jambo hili la kuhamasisha sensa na kumunga mkono Rais Samia Suluhu Hassan tulianza matembezi ya kawaida na kufuata na mazoezi ya viungo, “ alisema. Mwenyekiti wa Chama cha Michezo ya Taifa (CHAMIJATA), Rajabu Lulanga alisema wanaishuru serikali kwa kuandaa tamasha hilo ambalo limewakutanisha sanaa tofauti na michezo yote.

“Tunashukuru walioandaa tamasha hili wameonesha kuelewa jitihada za Rais Samia Suluhu Hassan katika maendeleo na jambo hili la sensa bila kuhesabiwa hakuna shughuli inayofanyika katika jambo lolote lile, “alisema.

Habari Zifananazo

Back to top button