Wadau wasifu miradi Tasaf, washauri kufanyia kazi dosari

WADAU wa maendeleo wameridhishwa wa miradi inayotekelezwa na Mfuko wa Maendeleo ya Jamii (Tasaf) na kushauri mfuko huo kufanyia kazi dosari zilizopo ikiwamo ucheleweshaji wa malipo kwa walengwa ili kusaidia kufi kia lengo la kupunguza umaskini nchini.

Akizungumza wakati wa ziara ya kufanya tathimini ya utekelezaji wa miradi ya Tasaf katika vijiji vya Itundwi na Bukulu wilayani Kondoa, Annie Homes kutoka Ubalozi wa Uingereza alisema wameona mambo mengi mazuri ambayo wanufaika wa mpango huo wamefanya katika kujikwamua kiuchumi.

“Katika ziara hii tumeona namna ambavyo walengwa wamefikiwa kupitia fedha za ruzuku ambazo wamekuwa wakipatiwa kujiongezea kipato kwa kuanza na kiasi kidogo cha fedha wanazopatiwa kufuga kuku, mbuzi na wengine kununua ng’ombe”. “Tumeridhika na namna ambavyo miradi hii inavyotekelezwa lakini tunapendekeza kwa Tasaf kuongeza jitihada katika kusimamia walengwa na kuondoa dosari ambazo zimejitokeza ikiwemo ucheleweshaji wa malipo ya walengwa ili kusaidia kufikia malengo ya kupunguza umaskini Tanzania,” alisema.

Advertisement

Aidha, Homes alisema kutokana na namna ambavyo walengwa wengi wamenufaika na mpango huo ipo haja kuanza kutolewa elimu ili wahitimu na nafasi zao kuchukuliwa na watu wengine wenye uhitaji. Naye Naiseku Kisambu kutoka Ubalozi wa Sweden alisema pamoja na mafanikio waliyoyapa walengwa wa mpango huo kupitia miradi mbalimbali bado ipo haja na kutilia mkazo suala la usawa wa kijinsia katika miradi ya Tasaf.

Alisema bado lipo tatizo katika maeneo mengi katika usawa wa kijinsia kwenye miradi ya Tasaf, hali ambayo inapaswa kutiliwa mkazo ili kuongeza ushiriki wa makundi yote na kufikia azma ya kupunguza umaskini bila kumwacha mtu nyuma.

Kwa upande wa Mkurugenzi wa Uratibu Tasaf, Haika Shayo alisema ziara hiyo imelenga kufanya tathmini ya utekelezaji wa miradi kwa walengwa wa kaya maskini. Ziara kama hii pia inaendelea katika mikoa ya Mtwara, Kilimanjaro na Dodoma ambapo timu zinakagua utekelezaji wa miradi ya mpango wa ajira za muda na kusikiliza maoni yao namna ambavyo walivyonufaika na kubaini changamoto walizonazo na kuzitafutia suluhu.

4 comments

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *