Wadau wataja ya kuzingatia marekebisho sheria ya ndoa

Wadau wataja ya kuzingatia marekebisho sheria ya ndoa

WIZARA ya Katiba na Sheria imeanza kukusanya maoni ya wadau na makundi mbalimbali kwa lengo la kufanyia marekebisho Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ili kuondoa ubaguzi kwenye umri wa chini wa ndoa kwa wavulana na wasichana.

Miongoni mwa wadau ambao wizara hiyo inaendelea kukutana nao ni Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria, wabunge, viongozi wa dini, viongozi wa kimila na waendesha bodaboda.

Kwa sasa timu ya wataalamu ipo katika mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Mtwara na Lindi.

Advertisement

Waziri wa Katiba na Sheria, Dk Damas Ndumbaro amebainisha hayo katika taarifa yake kwa umma jana.

Akirejea uamuzi wa Mahakama Kuu ya Tanzania mwaka 2016, Dk Ndumbaro alisema mahakama hiyo katika kesi ya Rebecca Gyumi dhidi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali katika Maombi Namba 5 ya 2016, ilitoa uamuzi kuhusu umri wa kuoa au kuolewa.

Alisema Mahakama Kuu iliamua kuwa Sheria ya Ndoa ipitiwe upya ili kuondoa ubaguzi na kukosekana kwa usawa kati ya umri wa chini wa ndoa kwa wavulana na wasichana.

“Mahakama ilisema kuwa Kifungu cha 13 na 17 cha Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971 ni kinyume cha Ibara ya 12, 13 na 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 ambayo inatoa haki sawa kwa wote mbele ya sheria,” alisema Dk Ndumbaro.

Alisema vifungu vya 13 hadi 17 vya Sheria ya Ndoa ya Mwaka 1971, vimebainisha kuwa mtoto wa kike anaweza kuolewa akiwa na umri wa miaka 14 kwa ridhaa ya wazazi au amri ya mahakama, hivyo kwa mujibu wa sheria hiyo, mtoto wa kike ni mtu ambaye hajafikisha umri wa miaka 14.

Alisema sheria hiyo pia inatenganisha umri wa kuoa kwa mtoto wa kiume na kuolewa kwa mtoto wa kike, ambayo mtoto wa kiume anatakiwa kuoa akiwa na umri wa miaka 18 na wa kike anatakiwa kuolewe akiwa na umri wa miaka 15 au pungufu kutegemeana na mazingira yaliyopo.

Katika hilo, wadau wa sheria wametaja mambo kadhaa ya kuzingatiwa katika marekebisho ya sheria ikiwamo umri wa mtu kuoa au kuolewa kutokuwa chini ya miaka 18.

Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Anna Henga, Ofisa Programu wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS), Mercy Kessy na Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wanahabari Wanawake Tanzania (TAMWA), Rose Reuben, wamesema umri wa kuoa au kuolewa unatakiwa uanzie miaka 18 na siyo chini ya hapo.

“Sheria ya sasa inamtaka mwanaume kuoa akiwa na umri wa miaka 18 ambao kikatiba ni mtu mzima, lakini kwa upande wa kuolewa umri ni tofauti ambapo sheria inaruhusu kuolewa na umri wa miaka 15, huyu binti anayeenda kuolewa bado mdogo kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania,” alisema Kessy.

Alivitaja vifungu vingine vyenye upungufu ni kifungu cha 13(2) ambacho kinaipa mahakama mamlaka ya kuruhusu kuoa au kuolewa kama wahusika wamefikisha umri wa miaka 14 wakati kifungu cha 17 kinataka kuwepo ridhaa ya wazazi ikiwa msichana hajafikisha umri wa miaka 18.

Reuben kwa upande wake alisema baadhi ya athari zinazowapata watoto wa kike kuolewa katika umri mdogo kutokana na sheria hiyo ni kupoteza fursa za elimu na ujuzi wa kazi na kupata maambukizi ya Virusi Vya Ukimwi (VVU) au magonjwa ya zinaa.

Alizitaja athari nyingine ni kunyanyasika kisaikolojia, kimwili, kijinsia, kufariki wakati wa kujifungua kwa kuwa viungo vyao vya uzazi havijakomaa, kuongezeka kwa vifo vya wajawazito na kuharibika kwa mimba.

Henga alitaja upungufu mwingine ni sheria kutaka migogoro ya ndoa ianzie kwenye mabaraza ya ndoa na ndipo iende mahakamani, lakini mabaraza hayo hayapo sehemu nyingi, hivyo kuzuia haki ya msingi ya talaka.

Add a comment

Toa Jibu

Barua-pepe haitachapishwa. Fildi za lazima zimetiwa alama ya *