Wadau wataka 10% za halmashauri zipelekwe benki

WADAU wa uchumi na jamii wameishauri serikali baada ya kusitisha utoaji mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu, mikopo hiyo iwe inapelekwa katika dirisha la mikopo benki na taasisi za mikopo zilizo katika halmashauri husika ili wao ndio wazitoe kwa kuwa wana utaalamu wa fani hiyo.

Hayo yamebainishwa jana kwa nyakati tofauti na wadau hao baada ya kauli ya  Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa aliyoitoa juzi bungeni Dodoma wakati akihitimisha mjadala wa hoja ya makadirio ya matumizi ya Ofisi ya Waziri Mkuu, taasisi zake na Mfuko wa Bunge kwa mwaka wa fedha 2023/24.

Katika hotuba yake, Majaliwa alihitimisha kwa kuzielekeza  halmashauri zote nchini kusitisha utoaji wa fedha za mikopo ya vikundi vya wanawake, vijana na watu wenye ulemavu zinazotokana na makusanyo ya kuanzia Aprili hadi Juni mwaka huu.

Alisema hatua hiyo imechukuliwa ili kuipa fursa serikali ya kujipanga kuwa na mfumo mpya wenye tija kutoa mikopo hiyo.

Akizungumzia hatua hiyo, msomi na mchambuzi wa masuala ya uchumi na jamii, Gabriel Mwang’onda alisema ni wazo zuri lakini limekuja kwa kuchelewa.

“Hili suala la asilimia 10 ya mikopo mara nyingi liligubikwa na sintofahamu nyingi. Tulishashauri jambo lifanywe na benki au taasisi za fedha ambazo wana watu wenye taaluma ya kujua taratibu za utoaji mikopo,” alisema Mwang’onda.

Alisema kwa kawaida mikopo haitolewi  tu na mtu yeyote na hali ilivyokuwa katika halmashauri nchini mikopo hiyo ilitolewa bila kuzingatiwa kanuni za mikopo na ndiyo maana kuliibuka malalamiko mengi ya walengwa kukosa na wengine mikopo ilitolewa kwa vikundi visivyojulikana.

“Nilipendekeza mikopo hii isitolewe na halmashauri, bali kila halmashauri ipeleke fedha hizo katika benki au taasisi za fedha katika halmashauri husika na ziwekwe kwenye dirisha la mikopo la benki wao ndio wahusike kuzitoa kwa kuwa wanajua taratibu za mikopo,” alisema Mwang’onda.

Alisema hatua ya Waziri Mkuu kutangaza kusitishwa kutolewa kwa mikopo hiyo ni njema na inaangaliwa namna mpya ya kutekelezwa kupitia mfumo wa benki na asasi za kifedha ili kuondoa malalamiko na fedha hizo kutopotea kwa vikundi hewa.

Mchambuzi wa uchumi na siasa na masuala ya jamii, Goodluck Ng’ingo alisema uamuzi wa Waziri Mkuu ni wa msingi katika kudhibiti upotevu wa fedha ambao Mkaguzi na Mdhibiti Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), amebainisha katika ripoti ya ukaguzi aliyotoa hivi karibuni.

Ng’ingo alisema dhumuni la mikopo hiyo kwa walengwa ilikuwa ni kuwapa mtaji lakini kutokana na mfumo wa utoaji, ilileta malalamiko na pia tija ndogo imechangiwa na uhaba wa watumishi wanaohusika katika halmashauri kushughulikia mikopo hiyo.

“CAG alibainisha katika ripoti yake upungufu wa utoaji wa mikopo hiyo, hivyo hatua iliyochukuliwa na serikali ni katika kudhibiti upotevu wa fedha usiendelee, lakini jambo la msingi sasa wazielekeze fedha hizo kwenye taasisi za kifedha kama benki ambao wana utaratibu wa utoaji mikopo,” alishauri Ng’ingo.

Alisema benki zina udhibiti mzuri zaidi wa utoaji mikopo na hivyo ni vyema serikali ikaangalia njia hiyo mbadala ya fedha hizo kupelekwa huko kwani hata sasa idadi ya watumishi wanaohusika na utoaji mikopo ni wachache na hawawezi kusimamia vizuri na tija ikaonekana.

Katika hatua nyingine, wabunge  wamepigilia msumari uamuzi wa serikali kusitisha mikopo ya asilimia 10 kwa vikundi vya wanawake, vijana na wenye ulemavu iliyokuwa ikitolewa katika halmashauri kwa kutaka waliohusika katika ubadhirifu wa fedha hizo wachukuliwe hatua.

Wakichangia makadirio ya mapato na matumizi kwa mwaka wa fedha 2023/2024 ya Ofisi ya Rais, Tamisemi yaliyowasilishwa na Waziri Angellah Kairuki, baadhi ya wabunge waliunga mkono maelekezo ya Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa halmashauri kusitisha mikopo hiyo kuanzia Aprili hadi Juni, mwaka huu.

Mbunge wa Viti Maalumu, Felister Njau (Chadema) alimpongeza waziri mkuu  kwa kufikia uamuzi huu na kusisitiza kuwa anaungana na serikali katika hilo.

Kwa upande wake, Stella Fiyao, (Chadema) alisema mikopo hiyo ilinufaisha wachache. Akirejelea Ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), alisema Sh bilioni 88 zimepotea, hazijulikani zilipo na hata vikundi havijulikani.

Habari Zifananazo

Back to top button