Wadau wateta ushiriki wa Watanzania miradi ya kimkakati

SERIKALI imesema hadi kufikia Desemba 2022 iliratibu programu 72 za uwezeshaji nchini zilizotoa mikopo yenye riba nafuu yenye thamani ya shilingi Trilioni 6.095 kwa wafanyabiashara zaidi ya milioni 8.6, ili kuwasaidia wananchi kushiriki na kufaidika na miradi ya kimkakati inayoendelea nchini.

Kauli hiyo imetolewa na Katibu Mkuu Wizara ya Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dk Hashil Abdallah leo Juni 26, 2023 jijini Dar es Salaam katika kikao cha wadau kujadili taarifa ya tathmini ya ushiriki wa Watanzania katika uwekezaji wa miradi ya kimkakati nchini kilichoandaliwa na Baraza la Taifa la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi (NEEC).

“Kwa muktadha huo, serikali imechukua hatua za makusudi zinazolenga kukuza ushiriki wa Watanzania na kuhakikisha kuwa miradi ya kimkakati na uwekezaji unanufaisha Watanzania kupitia ajira,” alisema.

Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa NEEC, Beng’i Issa, amesema ni wajibu wa sekta ya umma na sekta binafsi kukuza ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati inayoendelea nchini.

Amesema tangu mwaka 2015, ushiriki wa Watanzania katika miradi ya kimkakati na uwekezaji umekuwa ukiongezeka kupitia ajira kwa Watanzania, manunuzi ya bidhaa na huduma za ndani, ushirikishwaji wa jamii na uhawilishaji wa teknolojia katika seta zote za kiuchumi.

“Ili kuongeza ufanisi na tija kwa Watanzania kushiriki kikamilifu katika uwekezaji na miradi ya kimkakati tunahitaji kuwa na ushahidi wa kutosha kuhusu hali ilivyo sasa.

“Hii itawezesha serikali na sekta binafsi kuchukua jitihada za makusudi katika kuhakikisha kuwa Watanzania wanashiriki kikamilifu na wananufaika na thamani inayopatikana kutokana na uwekezaji na miradi ya kimkakati,” amesema.

 

 

Habari Zifananazo

4 Comments
Oldest
Newest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Back to top button